18 November 2011

Mabondia waachwa kwenye mataa

Na Amina Athumani

WASHIRIKI 30 wa kozi ya ukocha wa ngumi, ambayo ilipangwa kuanza jana mjini Kibaha wamejikuta wakiachwa kwenye mataa na kozi hiyo kuota mbawa, baada ya mkufunzi kutoka Aljeria kushindwa kutokea.


Kozi hiyo ambayo ilikuwa inahusisha makocha wa ngumi za ridhaa nchini, ilipangwa kufanyika katika Shule ya Sekondari ya Filbert Bayi, Kibaha chini ya Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC).

Makocha hao walijikuta kwenye wakati mgumu, baada ya kufika katika shule hiyo na kuambiwa na mwakilishi wa TOC, Mwinga Mwanjara ambaye alikuwepo eneo hilo kwamba kozi hiyo haitakuwepo kama ilivyopangwa, kwa kuwa mkufunzi waliyemtegemea hakuwez kufika.

Akizungumza kwa simu akiwa Kibaha, Makamu wa Rais wa Shirikisho la Ngumi za Ridhaa Tanzania (BFT) Michael Changarawe, alisema washiriki wote waliofika kuhudhuria mafunzo hayo, wamechanganyikiwa baada ya kutotaarifiwa kufutwa kwa kozi hiyo.

"Hadi hapa ninapozungumza na wewe (jana), watu wamechanganyikiwa na wala hatujui cha kufanya mara tunaambiwa kozi imefutwa, halafu mara mkufunzi kapata matatizo hatujui chakufanya," alisema Changarawe.

Changarawe alisema cha kushangaza, kozi hiyo ilikuwa ipo kwenye ratiba ya TOC na kabla ya mafunzo yao, tayari watu wa judo walifanya mafunzo kama hayo bila vikwazo.

Alisema cha msingi ni TOC kurejesha nauli za washiriki, ambao baadhi yao wametokea katika mikoa mbalimbali na BFT, haina uwezo wa kuwalipa kwa kuwa kila kitu kipo chini ya TOC.

Naye mpiga picha wa gaazeti hili Rajabu Mhamila 'Supe D', ambaye alikuwa mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo, alisema mchezo huo unaonekana kutopewa kipa umbele na ndiyo maana vitu kama hivyo vinatokea.

"Tunachotaka sisi ni kulipwa fedha zetu za nauli watu wa mikoani warudi na sisi tuendelee na shughuli zetu, hapa tulipo hata chai hatujanywa," alisema Super D.

Hata hivyo juhudi za kumpata mwakilishi wa TOC, Mwinga ambaye alikuwepo eneo la tukio hilo, zilishindikana.

Kozi hiyo ya ngumi, awali ilipangwa kufanyika Novemba 12 mwaka huu, lakini haikufanyika kutokana na mkufunzi wa mafunzo hayo kutoka Algeria, Azzedin Aggoune kupatwa na dharura.

Kutokana na hatua hiyo, BFT waliamua kuisogeza kozi hiyo hadi jana, ambayo pia haikufanyika.

No comments:

Post a Comment