Na Zahoro Mlanzi
HATIMAYE yametimia! Ndivyo unavyoweza kusema kwa wachezaji Haruna Moshi 'Boban' na Gaudance Mwaikimba, baada ya kuitwa katika kikosi cha wachezaji 28 cha timu ya Tanzania Bara (Kilimanjaro Stars), kitakachoshiriki michuano ya Kombe la Chalenji itakayoanza kutimua vumbi Novemba 25, Dar es Salaam.
Wachezaji hao, mara baada ya kuonekana kutopewa kipaumbele katika timu ya taifa (Taifa Stars), licha ya kwamba wanafanya vizuri katika timu zao lakini kuna wakati waliichezea timu hiyo, hivyo nafasi pekee iliyokuwa imebaki ni kuichezea Kili Stars, jambo ambalo linaweza kusaidia waitwe Taifa Stars.
Boban kwa nyakati tofauti amekuwa akiisaidia timu yake ya Simba, katika mechi mbalimbali na mpaka mzunguko wa kwanza ukimalizika ana mabao matatu na Mwaikimba wa Moro United, mpaka sasa ana mabao sita na amekuwa akitoa mchango mkubwa kwa timu hiyo.
Akizungumza Dar es Salaam jana wakati wa kutangaza kikosi hicho kwa niaba ya Kocha Mkuu, Charles Mkwassa, Kocha Msaidizi wa Kili Stars Jamhuri Kihwelu 'Julio', alisema timu hiyo itaanza kambi leo jijini Dar es Salaam na kwamba baada ya wiki moja atapunguza wanane na kubaki na 20.
“Timu itaingia kambini kesho (leo) katikati ya jiji kwenye hoteli ya Rainbow na kwamba tumechagua hoteli hiyo, tukiwa na maana yetu kwani uwezo wa kuhakikisha wachezaji wanakuwa na nidhamu wakati wote, licha ya kwamba tutakuwa mjini,” alisema Julio.
Aliwataja wachezaji hao na timu wanazotoka ni makipa Juma Kaseja (Simba), Deogratius Munishi (Mtibwa) na Shaaban Kado (Yanga), mabeki ni Shomari Kapombe, Juma Jabu na Juma Nyosso (Simba), Godfrey Taita (Yanga), Paul Ngelema (JKT Ruvu), Said Morad na Erasto Nyoni (Azam) na Salum Telela (Moro Utd).
Wengine ni viungo Shaaban Nditi (Mtibwa), Ibrahim Mwaipopo na Ramadhan Chombo (Azam), Nurdin Bakari (Yanga), Mwinyi Kazimoto (Simba), Rashid Yusuph (Coastal) na Jimmy Shogi (JKT Ruvu), washambuliaji ni Mohamed Sudi (Toto), Mrisho Ngassa na John Bocco (Azam).
Aliwataja wengine ni Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu (TP Mazembe), Nizar Khalfan (Vancouver), Hussein Javu (Mtibwa) na Daniel Reuben (Coastal).
Mbali na hilo, alitoa wito kwa Watanzania kujitokeza kwa wingi kuipa sapoti timu hiyo kwa kuwa jukumu hilo si la kwao pekee yao, bali ni la Watanzania wote ili mwisho wa siku watimize malengo yao.
“Michuano ikishaanza watu wajitokeze kuipa sapoti timu yao, kwani vita iliyopo mbele yetu ni yetu wote, kikubwa ni kujipanga kuhakikisha tunashinda na kulibakisha kombe nyumbani kama ilivyokuwa mwaka jana,” alisema Julio.
Akizungumzia kundi waliopo ambalo lina timu za Rwanda, Namibia na Djibouti, alisema soka ni kujipanga na pia hakuna timu ngumu wala rahisi, kinachotakiwa ni kujiandaa na kulibakisha kombe nyumbani.
No comments:
Post a Comment