Na Amina Athumani
MKUFUNZI aliyeteuliwa kuendesha kozi ya ngumi nchini na Shirikisho la Ngumi la Ridhaa la Kimataifa (AIBA), Azzedin Aggoune kutoka Algeria amewakera viongozi wa Shirikisho la Ngumi za Ridha Tanzania (BFT), kutokana na kushindwa kufika kwa wakati.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa BFT Makore Mashaga, alisema Mkufunzi huyo amewakera kutokana na kushindwa kufika kwa wakati na kuifanya BFT kuingia gharama za kuwahudumia washiriki wa kozi hiyo, waliofika tangu juzi.
Alisema awali kozi hiyo ilipangwa kufanyika Novemba 12 hadi Novemba 18, mwaka huu lakini Mkufunzi huyo aliomba kuongezewa muda kutokana na kupata dharura.
Mashaga alisema maombi hayo yalitumwa moja kwa moja kwa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), ambapo alipanga kuwasili nchini jana ili kuendesha mafunzo hayo.
Alisema kutokana na sababu hiyo BFT, iliamua kuisogeza mbele kozi hiyo hadi leo.
"Chakushangaza na kusikitisha Mkufunzi huyo, ametuma barua AIBA na kueleza kwamba hataweza kuja leo (jana) kwa ajili ya kuendesha kozi hii na badala yake atakuja Novemba 18 (kesho).
"Kitendo hiki kimetukera kwa sababu watu kutoka mikoani wameshakuja, tunaingia gharama ya kuwahudumia huku mafunzo yenyewe yakiwa hayajaanza," alisema Mashaga.
Alisema kutokana na barua hiyo iliyotumwa na AIBA, wameamua kuifanya kozi hiyo keshokutwa atakapowasili Mkufunzi huyo, ambapo kwa mujibu wa barua hiyo kutoka AIBA, atawasili kesho.
Mashaga alisema baadhi ya washiriki, ambao tayari wapo jijini tangu juzi ni kutoka Mwanza, Mbeya na Morogoro huku baadhi ya washiriki wengine wakiwarudisha ambao ni kutoka Pwani, Mtwara na Tanga.
No comments:
Post a Comment