Na Severin Blasio, Morogoro
MABONDIA wa ngumi za kulipwa mkoani Morogoro, Maneno William â'Chipolopolo' na Albert Mbena wanatarajiwa kupigana Desemba 2 mwaka huu katika pambano lisilo la ubingwa.
Pambano hilo la raundi nane la uzani wa kg.54, litachezwa katika Ukumbi wa Kinole Sokoni, Morogoro Vijijini.
Mratibu wa pambano hilo, Daudi Julian alisema mjini hapa jana kuwa maandalizi yanakwenda vizuri na kwamba mabondia wote wamethibitisha kupanda ulingoni siku hiyo.
"Maandalizi yanakwenda vizuri na mabondia wote wako katika mazoezi makali, kuhakikisha wanafanya vizuri siku hiyo," alisema.
Julian alisema lengo la pambano hilo ni kuendeleza mchezo wa ngumi mkoani Morogoro, pamoja na kuinua vipaji vya mabondia wake.
Alisema kabla ya pambano hilo, kutakuwa na mapambano ya utangulizi, ambapo mabondia kutoka Wilaya za Kilosa, Kilombero na Ulanga mkoani hapa watachapana.
Mratibu huyo alisema mapambano hayo, yatasindikizwa na burudani ya muziki wa kizazi kipya kutoka kwa msanii Shaban Said 'Shebby Gizzo' wa Morogoro.
No comments:
Post a Comment