30 November 2011

Marsh awatetea akina Mkwassa

Na Shufaa Lyimo

KOCHA Msaidizi wa Taifa Stars Silvester Marsh, amewataka Watanzania kuacha kuwatupia lawama makocha wa timu ya Kilimanjaro Stars, Charles Boniface na Jamhuri Kihwelu 'Julio' baada ya kuanza vibaya mashindano ya Tusker Chalenji, yanayoendelea Dar es Salaam.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mwishoni mwa wiki, Marsh alisema licha ya kuanza vibaya kwa timu hiyo, lakini bado ina nafasi ya kushinda kwenye mechi za mbele.

Alisema timu hiyo ilianza vibaya katika mchezo wake wa ufunguzi kutokana na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kuwapa makocha hao majukumu ya timu hiyo katika kipindi kifupi, kabla ya kuanza kwa mshindano hayo.

"Naomba Watanzania wasiwalaumu makocha kwa sababu ya makosa machache, bali waendelee kuwapa ushirikiano kwa kazi ngumu wanayoifanya," alisema Marsh.

Marsh alisema mashindano ya mwaka huu, yana ushindani wa hali ya juu hasa ikizingatiwa kuwa kila timu, imejipanga vizuri tofauti na mwaka jana.

"Mwaka jana timu nyingi zilikuwa hazijajiandaa, lakini mwaka huu kila timu inacheza kwa ushindani mfano, ukiangalia Somalia, Burundi na Djibouti hivi sasa zinacheza vizuri tofauti na msimu uliopita," alisema.

Alisema anawapongeza makocha hao kwa uchaguzi walioufanya, katika kikosi cha Kilimanjaro Stars kwa kile kitendo cha kuongeza sura mpya, ambazo zinakubalika na wadau wa soka hapa nchini.

No comments:

Post a Comment