Na Amina Athumani
BEKI wa kati wa timu ya Taifa (Taifa Stars), Nadir Haroub 'Canavaro', ameondolewa katika kikosi hicho baada ya kuumia kifundo cha mguu wa kulia wakati wa mazoezi.
Kikosi hicho cha Stars kinajiandaa na mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia dhidi ya Chad itakayochezwa Novemba 11, mwaka huu jijini N'Djamena.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Boniface Wambura alisema kwa mujibu wa Daktari wa Stars, Dk. Juma Mwankemwa, alisema mchezaji huyo hakuvunjika isipokuwa amepata mshtuko mkubwa wa kifundo hicho ambapo itamchukua wiki mbili kupona sawa sawa.
Naye Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Jan Poulsen amesema kutokana na hali hiyo Haroub hatakuwemo kwenye kikosi hicho kwa ajili ya mechi hiyo na ile ya marudiano ambayo itachezwa Novemba 15, mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Poulsen amesema kwa muda uliobaki hataita mchezaji mwingine kwa ajili ya kuziba pengo la Haroub, hivyo kwa sasa atabaki na kikosi cha wachezaji 21 alionao kambini hoteli ya New Africa.
Wakati huohuo, Wambura aliongeza msafara wa Stars utakaokwenda Chad utakaoongozwa na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF, Eliud Mvella.
Alisema timu hiyo inatarajia kuondoka majira ya saa 9 alasiri kwa ndege ya Kenya Airways kupitia Nairobi ambapo watawasili N'Djamena saa 1 jioni ambapo kwa saa za Tanzania itakuwa saa 3 usiku.
Alisema timu hiyo itarejea nchini Novemba 12, mwaka huu kwa ndege ya Ethiopian Airlines na kwenda moja kwa moja kambini kujiandaa kwa mechi ya marudiano.
No comments:
Post a Comment