07 November 2011

Gama: Wataalamu wa kilimo msikae ofisini

Na Florah Temba, Moshi

MKUU wa Mkoa wa Kilimanjaro Bw. Leonidas Gama, amewataka wataalamu wa Kilimo mkoani humo, kuacha tabia ya kukaa ofisini badala yake waende kwa wakulima kuwapa utalamu ili waweze kujikomboa katika lindi la umaskini kupitia sekta hiyo.
Bw. Gama aliyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati akizungumza na viongozi mbalimbali wakiwemo Wakuu wa Wilaya, Makatibu Tawala, Wakurugenzi wa Halmashauri na wataalamu wa idara mbalimbali katika majumuisho ya ziara yake mkoani humo.

Alisema wataalamu wa kilimo na ufugaji hawana utamaduni wa kuwatembelea wakulima badala yake wanakaa ofisini hali ambayo inasababisha wakulima kujihusisha na kilimo cha mazoea.

“Hali ya kilimo katika Mkoa huu si mbaya sana lakini hali hii si kwamba inatokana na juhudi za wataalamu wetu wa kilimo hapana bali ni kutokana na wananchi wenyewe.

“Naomba kuanzia sasa, muende kwa wakulima ili waweze kulima kitaalamu na kupata mazao mengi hivyo kujikwamua kiuchumi,” alisema Bw. Gama.

Akizungumzia hali ya ufugaji mkoani humo, Bw. Gama alisema wananchi bado hawajanufaika na ufugaji kwani zipo changamoto nyingi ambazo zinaelezwa na wafugaji ikiwemo ukosefu wa chakula na ardhi ya malisho hali ambayo inasababishwa na wataalamu katika sekta hiyo kukaa ofisini.

Alisema wastani wa uzalishaji maziwa mkoani humo ni kati ya lita sita hadi nane ambao ni mdogo mdogo ukilinganisha nahali halisi ya mahitaji kwani wataalamu hao, wameshindwa kutoa mbinu mpya za ufugaji wa kitaalamu.

“Inaonesha kabisa wataalamu wetu wanakaa ofisini, hawaendi kwa wananchi kuwapa utaalamu, lazima wabadilike ili tuweze kuwakomboa wananchi na umaskini,” alisema

Alisema wataalamu hao wanapaswa kwenda kwa wananchi ili kutatua matatizo yao pamoja na kuwapa mbinu za kitaalamu juu ya kilimo na ufugaji ambazo zitawawezesha kufuga mifugo michache na kupata faida kubwa badala ya kufuga mifugo mingi wakati hakuna eneo la malisho.

Mwisho.
7777777

FORTH

'Wazazi anzisheni vikundi, kubuni miradi'
Na Rose Itono

WAZAZI wameshauriwa kuanzisha vikundi na kubuni miradi mbalimbali ambayo itasaidia kutoa ajira kwa vijana na kuwapunguzia muda wa kukaa vijiweni.

Wito huo umetolewa Dar es Salaam mwishoni mwa wiki na Mwenyekiti wa Chama cha Kusaidiana cha Wanawake kilichopo Goba, Manispaa ya Kinondoni (KIWAKUKI) Bi. Regina Maziku, katika hafla ya kuchangia mfuko huo.

Alisema kama wazazi wataanzisha vikundi na kubuni miradi ya maendeleo, itasaidia kuongeza ajira za vijana badala ya kukaa vijiweni na kufanya mambo yasiyofaa.

Aliongeza kuwa, hadi ssa chama hicho kina miradi mbalimbali ukiwepo wa mapishi na upambaji ambayo huwachukua vijana na kuwalipa.

“Kila tunapopata tenda tunachukua vijana ili waweze kujipatia pesa ambazo huwasaidia kutatua matatizo yao,” alisema Bi. Maziku na kuongeza kuwa, chama hicho pia kinawatumia wataalamu wa mifugo ili kuwafundisha wanachama wao ufugaji kuku wa kienyeji kisasa ili kuongeza kipato chao.

Aliwataka viongozi wa Serikali kushirikiana na vyama hivyo kwa kupeana mafunzo mbalimbali ili waweze kupata maendeleo na kupunfuza utegemezi.

Mwisho.
THIRD

GRL wapanda zaidi ya hekta 14,000 za miti 

Na Mercy James, Mufindi

ZAIDI ya hekta 14,660 za miti ya mbao zimepandwa katika Kata ya Makungu na Kiyowela Wilaya ya Mufindi Mkoani iringa katika kipindi cha mwaka 2005 hadi mwaka huu.

Miti hiyo imepandwa na kampuni ya upandaji miti ya Green Resources Limited
(GRL) ambayo ipo chini ya kampuni Tanzu ya shirika mama la Tree farm A/S kutoka nchini Norway.

Akisoma risala katika hafla za kufunga mpando Meneja mradi wa GRL Bw. Alon Raiza, alisema shirika hilo lilitekeleza mradi huo wa upandaji miti baada ya kuombwa na wananchi wa vijiji viwili na kwamba kwa upande wa Makungu kilitoa hekta 2,500 na eneo la bustani lenye ekali 12 huku Idete ikiwa imetoa heklta 11,660.

Bw.Raiza alisema lengo la kuanzisha miradi katika vijiji hivyo ni kuzalisha mazao ya misitu kama vile Mbao, nguzo na utunzaji mazingira, kuhifadhi uoto wa asili na kupunguza hewa kukaa angani pamoja na kusaidia jamii kuinua uchumi hususani vijiji vya wilaya hiyo.

Mgeni rasmi katika sherehe hizo Mkuu wa Wilaya ya Mufindi Bi. Evarista Kalalu, aliwataka wananchi wa vijiji hivyo kutumia vema fursa hiyo kwa kupanda miti kwa wingi ili kuwekeza katika misitu.

Bi. Kalalu alisema wananchi wanaopuuza mradi huo wanapaswa kujirekebisha na kwamba hizo ni dalili za uvivu wa kufikiri na kuwataka kupanda miti kwa manufaa ya watoto wao na kizazi kilichopo na kijacho.

Alisema Wilaya inahitaji wananchi wanaojituma katika kutekeleza shughuli za maendeleo na si kusubiri kufanyiwa kila jambo na kwamba soko la mazao yatokanayo na misitu ikiwemo uuzaji wa hewa ukaa si hadithi na kwamba waitumie ardhi waliyo nayo kupanda miti kama vichaa ili kuinua uchumi wao na wa taifa.

“Wekezeni katika ardhi rasilimali ambayo ni zawadi kutoka kwa mwenyezi Mungu, mkikaa watakuja wajanja watawekeza alafu mtakuwa watumwa wa wageni, na hao watoto wenu mtashindwa kitu cha kuwaonesha siku za usoni,”alionya kiongozi huyo.

Upande wake Meneja mkuu wa GRL Bw. Sangito Sumari, alisema katika mradi huo jumla ya wananchi 250 hadi 450 hujipatia ajira za msimu na ajira za kudumu pamoja na kushiriki shughuli za maendeleo kama kujenga madarasa.

Alisema mbali ya miradi ambayo imekwisha kutekelezwa miaka iliyopita kabla ya kumaliziak kwa mwaka huu GRL inatarajia kuanza ujenzi wa Zahanati  katika kijiji cha Lole ikifuatiwa na ukumbi wa kijiji cha Makungu na Ofisi ya Kijiji cha Kiyowela na kumalizia daraja dogo la Igologolo.

Awali mkuu wa Wilaya hiyo alipata fursa ya kutembelea vitalu na moja ya shamba la mbegu ya miti kutoka Nairobi nchini Kenya yenye sifa za kukua kwa haraka tofauti na mbegu nyingine zilizopo nchini na kwamba mbegu hiyo  imeletwa kwa ajili ya majaribio.
mmwisho.

LEAD

'Ulipaji ada kwa wakati ni changamoto kubwa shule binafsi'

Na Anneth Kagenda

CHANGAMOTO kubwa inayozikumba shule zisizomilikiwa na serikali ni wazazi kuchelewa kulipa ada na michango mbalimbali kwa wakati hivyo kusababisha uendashaji kuwa mgumu, imeelezwa.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Dar es Salaam mwishoni mwa wiki kwenye mahafari ya nne ya darasa la saba Mwalimu wa shule ya Msingi Rightway Bw. Moses Kyando, alisema hiyo ni moja ya changamoto kubwa wanayokumbana nazo.

Alisema pamoja na kwamba shule zisizo za serikali zimekuwa zikitumia nguvu kubwa kutoa elimu bora na kufaulisha wanafunzi lakini wazazi wamekuwa ni kikwazo kikubwa katika ulipaji wa ada za watoto wao kwa wakati.

"Ni kweli shule hizi zinajitahidi kutoa mafunzo kwa bidii lakini wazazi wamekuwa wakitukwamisha inapofika wakati wa kulipa ada, lakini pia changamoto nyingine ni wanafunzi kushindwa kuendelea na masomo kutokana na hali ya uchumi ya wazazi wao,"alisema.

Alisema kutokana na kupanda kwa gharama za uendeshaji na serikali kutotoa ruzuku kwa shule hizo wakati mwingine ada huwa kubwa kiasi hivyo wazazi wengine wamekuwa hawawezi kuhimili kulipa hivyo kusababisha watoto wao kutoendelea na shule huku wengine wakihama hama kutokana na wazazi wao kubadilisha makazi," alisema Bw. Kyando.

Aliwashauri wazazi kutambua umuhimu wa kuwalipia watoto wao ada kwa wakati ili kuepusha shule hizo na wakati mgumu na kusisitiza kuwa kuchelewesha ada ni kukwamisha wanafunzi kupata elimu nzuri na katika hali inayotakiwa.

Kwa upande wake Mgeni rasmi katika mahafali hayo Bw. Hassan Kalinga, ambaye ni Ofisa Elimu wa Manispaa ya Kinondoni aliahid kuwa Ofis yake itashirikiana na shule za binafsi kuhakikisha kiwango cha elimu kinakuwa na kupata ufaulu wa wanafunzi wengi zaidi.

No comments:

Post a Comment