16 November 2011

Amuua mdogo wake kwa ahadi ya pikipiki

Na Esther Macha, Mbeya

MKAZI wa Kijiji cha Mpanda, Kata ya Nyimbili, Wilaya ya Mbozi, mkoani Mbeya, Bw. Iman Kalinga (22), anadaiwa kumuua mdogo wake
na kumnyofoa baadhi ya viungo kama ulimi, moyo na sehemu za siri baada ya kuahidiwa pikipiki yenye thamani ya sh. milioni moja.

Tukio hilo limetokea Novemba 14 mwaka huu, saa 10 jioni kijijini hapo ambapo mtuhumiwa anadaiwa kumuu Bw. Heron Kalinga (17).

Akizungumza na Majira jana, Ofisa Mtendaji wa kijiji hicho Bw. Nelbert Shonza, amethibitisha kutokea kwa mauaji hayo na kuongeza kuwa, baadhi ya watu wanaodhaniwa kuhusika na tukio hilo wanashikiliwa na Jeshi la Polisi akiwemo mfanyabiashara maarufu wa eneo la Ilolo, wilayani humo.

“Baada ya tukio hili, mtuhumiwa alinusurika kupigwa na wananchi wenye hasira lakini nilimuokoa, mtumuhiwa alitoa ushirikiano wa kuwataja watu waliomtuma na walioshirikiana kumuua mdogo wake,” alisema Bw. Shonza.

Kamanda wa Polisi mkoani humo, Advocate Nyombi, alikiri kuwepo kwa tukio hilo na kusema ufafanuzi zaidi utatolewa na Mkuu wa Upepelezi wilayani humo.

No comments:

Post a Comment