Na Esther Macha, Mbeya
MKUU wa Wilaya ya Mbeya Bw. Evance Balama, amemuagiza Kamanda wa Polisi na Mkuu wa usalama barabarani mkoani humo kuwathibiti na kuwachukulia hatua kali askari wanaodaiwa kuyalinda magari ya abiria yanayolalamikiwa na wananchi pindi yanapofanya makosa kwa maslahi yao binafisi.
Bw. Balama alitoa agizo hilo jana baada ya kuibuka kwa malalamiko ya baadhi ya wamiliki wa vyombo vya usafiri wa abiria mkoani hapa wakiwatuhumu askari wa usalama barabarani kufanya kazi kwa upendeleo kusimamia sheria kwa kushindwa kuwachukulia hatua baadhi ya magari yanayofanya makosa ya wazi.
Wakizunguzma katika semina ya watumiaji huduma za usafiri wa majini na nchi kavu, ulioandaliwa na baraza la ushauri la Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA -CCC), wamiliki na wadau wa hao walilishutumu kikosi cha usalama barabarani la jeshi la polisi Mkoa wa Mbeya kwa kushindwa kusimamia ipasavyo sheria bila upendeleo.
Walisema wamekuwa na tabia ya kulindana kwa kutokamata magari yanayomilikiwa na polisi wenzao au wao wenyewe huku wakiwaonea magari ya rai wasiowajua.
Akijibu malalamiko hayo bw. Balama alisema kitendo hicho kinachofanywa na askari hao wa usalama barabarani ni kinyume na maadili ya utumishi wa umma kwa kuwa sheria zinapaswa kusimamiwa bila kujali wadhifa, madaraka wala nafasi za watu fulani ndani ya jamii.
“Kwanza ngoja nikwambie, hata kama mimi mwenyewe (Balama) nikivunja sheria ninapaswa kuchukuliwa hatua, si sahihi askari hao kuacha magari yao na yale ya askari wenzao yakiendelea kuvunja sheria bila kusimamiwa,”alisema.
Mkuu huyo wa wilaya alisema kutokana na malalamiko hayo tayari ameandaa mpango maalumu wa kupokea taarifa za siri ambazo zinawataja askari wanaojihusisha na upendeleo kwa kushindwa kuyakamata magari yao na yale ya wenzao yanapovunja sheria za usalama barabarani.
Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Baraza hilo la ushari SUMATRA -CCC Bw. Oscar Kikoyo, aliwataka watumiaji wa huduma za usafiri nchini kuhakikisha wanatimiziwa haki zao zote kwa kuwabana wamiliki wa vyombo hivyo.
Alisema ili kujenga jamii ya wastaarabu katika sekta ya usafirishaji nchini lazima abiria wapewe haki zao za msingi kama kupewa taarifa, kukubali, kuchagua na huduma bora.
Pia aliwataka wamiliki wa vyombo vya usafiri nchini kushauriana na wadau katika kutoa huduma bora badala ya wafanyabiashara hao kung’ang’ania kupata faida kubwa huku walaji (watumiaji) wakiendelea kunyanyaswa.
No comments:
Post a Comment