05 October 2011

Waziri: Wanaotesa wanyama sasa watawachukulia hatua

Na Rachel Balama

SERIKALI itawachukulia hatua za kisheria wasafirishaji mifugo na kuwalipisha faini ya sh. 20,000 hadi sh. 100,000 kama watakiuka sheria ya ustawi wa wanyama kwa
kuwafanyia vitendo vya ukatili.

Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. David Mathayo aliyasema hayo Dar es Salaama jana wakati akizindua maadhimisho ya siku ya wanyama duniani katika Viwanja vya Mnazi Mmoja.

“Wasafirishaji mifugo wanakiuka sheria ya ustawi wa wanyama kwa kuwafanyia vitendo vya ukatili wanapowasafirisha na kuwaona hawana thamani,” alisema.

“Natoa wito kwa wasafieishaji, wazingatie sheria na kuepuka kuwafanyia ukatili, atakayekiuka sheria hii atalipa faini, katika kuelekea miaka 50 ya uhuru, takwimu zinaonesha sekta ya mifugo  imepiga hatua katika kuongeza mapato ya taifa,” alisema.

Dkt. Mathayo, aliwataka wananchi kutunza mifugo, kuipatia mahitaji muhimu yanayostahili ina chakula ili kuongeza ustawi wa wanyama.

Katika maadhimisho hayo Dkt. Mathayo alizindua nembo mpya ya Chama cha Kutetea Haki za Wanyama nchini (TSPCA), tovuti na kutoa vyeti kwa washiriki wa warsha iliyohusu ustawi wa wanyama.

Pia alikabidhi cheti na fedha taslim sh. 500,000 kwa Mwandishi wa habari wa kituo cha televisheni cha ITV, Bw. Godfrey Monyo kwa kuandika habari zinazohusu wanyama kwa kina.

Mwenyekiti wa  TSPCA, Dkt. Sinare Sinare, alisema wamekuwa watetezi wa haki ya ustawi kwa wanyama tangu mwaka 1935.

“Tutahakikisha tunatoa elimu kwa umma kuhusu ustawi wa wanyama, ushawishi na utetezi kwa Serikali, kutoa huduma kwa wanyama na kufanya ukaguzi kwa kushirikiana na wizara husika.

No comments:

Post a Comment