Na Mwandishi Wetu
TIMU ya taifa 'Taifa Stars, inatarajia kuagwa kesho kwa ajili ya safari yao ya kwenda mjini Marrakech, Morroco kukamilisha mchezo wa mwisho wa Kundi D wa
kuwania kufuzu Mataifa ya Afrika, mwakani (CAN 2012).
Fainali hizo zitafanyika katika nchi za Guinea ya Ikweta na Gabon, ambapo kundi hilo linaongozwa na Morocco na Jamhuri ya Afrika ya Kati zikiwiana kwa pointi nane zikifuatiwa na Taifa Stars na Algeria zenye pointi tano kila moja.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Boniface Wambura alisema timu hiyo itaagwa saa 4 asubuhi kambini kwao jijini Dar es Salaam.
"Timu itaagwa asubuhi na siku hiyo hiyo mchana itakwenda jijini Casablanca na baadaye mjini Marrekech, kwa ajili ya mechi dhidi ya timu ya taifa ya Morocco," alisema Wambura.
Alisema mechi hiyo itapigwa Jumapili na kwamba tayari wachezaji watano wanaocheza nje ya nchi, wamesharipoti kambini.
Aliwataja wachezaji hao ni Idrissa Rajab anayechezea Sofapaka ya Kenya, Mbwana Samata (TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo- DRC), Henry Joseph (Kongsvinger IL, Norway), Nizar Khalfan (Vancouver Whitecaps, Canada) na Athuman Machupa (Vasalund IF, Sweden).
Aliongeza wachezaji wengine wanaocheza Vietnam, Abdi Kassim na Dan Mrwanda wao wanatarajia kuwasili nchini leo mchana majira ya saa nane.
Katika hatua nyingine, Wambura alisema Kamati ya Mashindano ya TFF, itakuwa na kikao na viongozi wa klabu zote 18 za Ligi Daraja la Kwanza, ambacho kitafanyika Oktoba 10 mwaka huu.
Alisema ligi hiyo itakayoanza Oktoba 15, mwaka huu itashirikisha timu za AFC ya Arusha, Burkina Faso ya Morogoro, Majimaji ya Ruvuma, Mbeya City Council ya Mbeya, Mgambo Shooting ya Tanga, Mlale JKT ya Ruvuma na Morani ya Manyara.
Zingine ni Polisi ya Dar es Salaam, Polisi ya Iringa, Polisi ya Morogoro, Polisi ya Tabora, Rhino Rangers ya Tabora, Samaria ya Singida, Small Kids ya Rukwa, Tanzania Prisons ya Mbeya, Temeke United ya Dar es Salaam na Transit Camp ya Dar es Salaam ambazo zitawekwa katika makundi matatu.
Aliongeza majimaji na Small Kids, ndizo pekee ambazo bado hazijalipa ada ya ushiriki ya sh. 200,000 na kwamba zimetakiwa kulipa ada hiyo kabla ya Oktoba 10, mwaka huu ambayo ndiyo siku ya kupanga ratiba.
No comments:
Post a Comment