Na Mwandishi Wetu
KAMPUNI zilizofutiwa leseni za kuuza sukari, zimesema Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Profesa Jumanne Maghembe amekiuka misingi ya sheria kwa kutolea
uamuzi jambo linalohusu mkataba kati ya pande mbili ambazo yeye si mmoja wao.
Taarifa iliyotolewa Dar es Salaam jana na kusainiwa na Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni ya Mohamed Enterprise, Bw. Gulam Dewji, ilisema uwakala wao wa kuuza sukari unatokana na mikataba kati yao na kiwanda cha Sukari TPC Limited.
“Mikataba yetu ina masharti ambayo kama yangekiukwa, kungekuwa na uhalali wa kuchukua hatua za kisheria zinazostahili,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo na kuongeza kuwa, uamuzi wa Prof. Maghembe haikuzingatia haki ya kusikilizwa.
Alisema kazi hiyo wameifanya kwa miaka 15 kwa umahiri na ufanisi mkubwa hivyo wanaiomba Serikali iwasikilize kwanza ili kupata picha kamili na kufanya maamuzi ya haki.
Taarifa hiyo iliongeza kuwa, wana mikkati mizuri ambayo tayari inaonesha mafanikio pamoja na kukutana na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro ili washirikiane mawazo kuhusu wafanyabiashara wasio waaminifu.
“Hatujapeleka sukari nje ya nchi, tunapowauzia wafanyabishara wa ndani, tunatarajia wauze ndani ya nchi sasa kama wanauza nje hilo ni jukumu la Serikali kujua nani alipeleka huko.
“Tumekuwa tukiuza sukari kwa kutumia vitabu vya risiti na tunatoa taarifa kwa maofisa biashara, katika vitabu hivyo hakuna kampuni ya Kenya au nchi nyingine,” ilisema taarifa hiyo.
Alisema suala la sukari kuuzwa nje ya nchi ni kuzibebesha kampuni hizo mzigo usio wa kwao kwani jukumu la kuthibiti mipaka ili sukari isiuzwe nje ya nchi ni la vyombo vya dola.
Aliongeza kuwa, Serikali inapaswa kuwadhibiti wafanyabiashara wadogo ambao pengine wananunua mifuko miwili miwili kutoka kwa mawakala wakubwa na kuiuza nje ya nchi kwa njia zisizo rasmi.
Alisema Serikali inapaswa kuwasaidia mawakala wakubwa ili kuzuia bidhaa hiyo isivushwe nje lakini siyo kuwaadhibu watu wanaofanya kazi kwa uadilifu na kuiomba Serikali kutazama upya uamuzi wake.
Akizungumzia bidhaa hiyo kuuzwa sh. 2,000 hadi sh. 2,500 kwa watumiaji majumbani, alisema wasambazaji hawahusiki kwa namna yoyote kwani hawajawahi kuuza rejareja na mawakala wanaouziwa wanafanya hivyo kwa bei iliyokubalika na sio vinginevyo.
Mwishoni mwa wiki Prof. Maghembe alitangaza kuzifutia leseni kampuni tatu za Staways Investment, Marenga Investment na Mohammed Enterprises kwa madai ya kuuza sukari kwa njia ya magendo na kusababisha bei ya bidhaa hiyo kupanda nchini.
serikali ijutie makosa yake ya kuwabinafshia wagabachori viwanda vya sukari huku wasabazaji waliopewa jukumu la usafirishaji ni hao hao. kesi ya nyani usimpe tumbili kuhukumu wote ni wakwea miti na maisha yao ni kwenye miti.
ReplyDelete