24 October 2011

Walimu wakuu sekondari 'wamkaba' koo Mkurugenzi

Na Eliasa Ally, Iringa

WAKUU wa Shule za Sekondari 27 katika Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Vijijini,, wamelelemikia Mkurugenzi wa
Wilaya, Bi.  Tina Sekambo, kwa kuzuia fedha ambazo zilishaingizwa katika akaunti za kila
shule kwa ajili ya ununuzi wa vitabu.

Walimu hao walidai kuwa hatua hiyo iliathiri shughuli za maandalizi ya mitihani ya kidato cha nne.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, kwa masharti ya majina yao kutochapishwa gazetini, walidai fedha hizo ni ruzuku za kutoka serikalini na zililenga sekondari za Wilaya ya Iringa.

Mmoja wa walimu hao alisema fedha hizo ziliingizwa kwenye akaunti za shule kati ya Juli na waliwataka wazitumie kununua vitabu vya kujifunzia na kufundishia.

Alidai kuzuiwa kwa akaunti hizo,kumechangia shughuli za sekondari yakiwemo  maandalizi ya mitihani ya kidato cha nne iliyomalizika hivi karibuni kukwama.

Walidai wakati fedha hizo zinatumwa kwenye akaunti za shule, kulikuwa na fedha zingine ikiwemo michango mingine.

"Kwa kweli sekondari zote za wilaya ya Iringa, tumepata shida makubwa,
baadhi ya wakuu wa sekondari tayari pesa hizo walishazitumia na wengine ilikuwa bado, lakini akaunti zote zilizuiwa na  kusababisha uendeshaji wa shule kuwa mgumu zaidi," alilalamika mwalimu mwingine.

Ofisa Elimu wa Sekondari wa Wilaya ya Iringa Vijijini, Bw. William Mkangwa, akizungumzia kuhusu malalamiko hayo, alisema yeye hawezi kuzungumzia suala hilo bali wenye uwezo ni Idara ya Uhasibu na mkurugenzi mwenyewe.

Akizungumzia suala la kuzuiwa akaunti za sekondari, Meneja wa Benki ya NMB Tawi la
Mkwawa, Bw. Atupele Mwakibete, alikiri kupokea barua ya Mkurugenzi wa Iringa Vijijini ya kumtaka azuie fedha za sekondari zisichukuliwe kutokanana sababu ambazo zipo chini ya mamlaka yake.

Bw. Mwakibete alisema Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, Bw. Sekambo anayo mamlaka ya kuzuia akaunti za idara zilizopo kwenye wilaya yeke fedha zisichukuliwe.

Mkuu wa Idara ya Uhasibu wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Vijijini, Bw, Mbiaji
Joseph, alikataa kuzungumzia suala hilo.

Bi. Sekambo alipotafutwa ili
kuzungumzia suala hilo hakupatikana kwani taarifa zilieleza kuwa yupo nje ya ofisi kikazi.

No comments:

Post a Comment