01 November 2011

Wabunge wahoji upotevu wa mamilioni Bodi ya Mikopo

*Kamati ya Mrema yakataa mahesabu halmashauri 3

Na Salim Nyomolelo

KAMATI ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) imeitaka Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HELB) kufuatilia
upotevu wa sh.milioni 150 kwa ajili kuwalipia wanafunzi mikopo.

Hoja hiyo ilitolewa na jana na mjumbe wa Kamati hiyo Bi.Ester Bulaya, katika kikao cha kamati hiyo Ofisi ndogo za Bunge Jijini Dar es Salaam na kuutaka taasisi hiyo kufanya uchunguzi kujua iwapo wahusika waliotakiwa kupata mkopo kwa kutumia fedha hizo walipewa baada ya wizi huo kutokea.

Mbunge huyo alisema licha ya Bodi hiyo kutoa kipaumbele kutoa mikopo kwa wanafunzi masikini lakini bado mikopo hiyo haiwafikii kundi hilo na kwamba wao kaama wawakilishi wa wananchi wanapewa kero hizo na wahusika.

"Nina ushahidi wa mtoto wa kigogo alipata mkopo huku mtoto wa masikini ambaye natoka naye katika kijiji kimoja alikosa,na bodi mnafahamu,"alisema
mbunge huyo.

Mjumbe mwingine wa kamati hiyo Bw.Alphaxard Ligora, alisema matatizo yanatokana na bodi yenyewe hivyo kusababisha migomo kwa wanafunzi kutokana na kufanya kazi kinyume cha sheria ambazo zilitungwa na Bunge.

Alisema wanakabiliwa na changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na kuchelewesha fedha vyuoni mara kwa mara na kwamba bodi hiyo ilikuwa na matumizi makubwa ya fedha za umma na yenye majina mengi na malipo mengi katika vikao vyao.

"Matumizi ni makubwa mno, nilivyoangalia natamani hata kulia mheshimiwa mwenyekiti," alisema mbunge huyo.

Katika majibu yake Mkurugenzi wa Bodi hiyo Bw.George Nyatega, alisema tayari kesi ya wizi wa fedha hizo ipo mahakani na kudai kuwa wizi huo haujaathiri utoaji wa mikopo kwa wanafunzi.

Mkurugenzi huyo alisema matatizo yanayoendelea katika utoaji mikopo ni kwa sababu huduma hiyo ilipoanzishwa haikuwa na miundombinu ya kutosha katika kujua uwezo wa fedha kwa mwombaji na kuongeza kuwa ukosefu wa vitambulisho vya taifa ndio chanzo kwa sababu vingeeleza taarifa sahihi za mwombaji.

3 comments:

  1. Upo udhaifu mkubwa sana katika uongozi wa nchi hii. Wizi unaojitokeza katika serikali kuu na serikali za mitaa, mashirika ya umma n.k. umekuwa unafumbiwa macho. Hii bila shaka inatokana sio tu na udhaifu wa viongozi bali pia viongozi wengi ni wabadhirifu. Kutowanyima watoto wa maskini mikopo na kuwapa wale wanaojiweza ni moja wapo ya matendo yanayojenga tofauti kubwa kati ya walio nacho na wasio nacho.Amani na utulivu haviwezi kudumu katika hali ya namna hii, kwani wale wanaoonewa siku moja watadai haki zao, na ole wa hao waonevu.

    ReplyDelete
  2. Jamani wanaipeleka wapi hii nchi? Mbona hawatambui kwamba kila kitu kina mwisho? Waangalie Misri, Tunisia na Libya. Mambo yalianza hivi, lakini kelele za wananchi zikapuuzwa. Wamekuwa vipofu na viziwi au ndio kulewa madaraka? Kila kitu kina mwisho wake.

    ReplyDelete
  3. Haya yaliposemwa na wabunge wa upinzani akiwemo Suzan Lymo, majibu yalikuwa
    "Huu ni uzushi na upotoshaji wa nia nzuri ya serekali"
    Sasa yameumbuliwa na kamati. Ngoja tuone kama kuna hata mmoja atawajibishwa au kujiuzulu kwa manufaa ya umma.

    ReplyDelete