10 October 2011

Sitta ataka wachezaji wasitumie dawa

Na Amina Athumani

WAZIRI wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samwel Sitta amewataka wanamichezo wa ukanda huo kuifanya Afrika Mashariki kuwa yenye wachezaji wasiotumia dawa za
 kuongeza nguvu michezoni.
Akizungumza katika Uwanja wa ndani wa Taifa, Dar es Salaam jana wakati wa uzinduzi wa mashindano ya mpira wa kikapu ya Kanda ya Tano Waziri Sitta, alisema kumekuwa na matukio mengi ya wachezaji kunywa dawa za kuongeza nguvu, kabla ya mchezo kuanza na kwamba hiyo itaondoa hadhi ya wachezaji endapo watashawishika kufanya hivyo.

"Tanzania tunapenda ushindani sana, lakini si ushindani wa kuongeza nguvu kwa dawa, wakati wa mechi tumeona matukio ya wanamichezo kama wanariadha, wachezaji wa soka wakikumbwa na kashfa ya kunywa dawa za kuongeza nguvu.

"Nawaomba ninyi kama wawakilishi wa ukanda huu kuifanya Afrika Mashariki kuwa ni ukanda usiokuwa na matumizi ya dawa za kumwongezea nguvu mchezaji katika kiwango chake," alisema Waziri Sitta.
Mashindano hayo ambayo yanashirikisha nchi saba kutoka katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, imekusanya wachezaji 300 ambapo kati ya hao wapo wanaowakilisha timu za wanawake na wengine wanaume.

Kwa upande wa Tanzania inawakilishwa na timu nne, ambazo ni Savio, Vijana, ABC na Jeshi Stars huku Kampuni ya vinywaji baridi ya Coca-Cola kupitia soda ya Sprite inadhamini michuano hiyo.

Katika mechi za ufunguzi jana kwa upande wa wanawake Tanzania ilianza vyema michuano hiyo, ambapo Jeshi Stars iliibuka na ushindi wa pointi 71-48, dhidi ya timu ya Ethiopia (Govern House Agency).
Awali kulifanyika mechi kati ya Berco Stars ya Burundi na KCC ya Kenya ambapo KCC ilichomoza na ushindi wa pointi 56-40.
Nchi zinazoshiriki mashindano hayo ni Kenya, Uganda, Burundi, Ethiopia, Sudan Kusini, Zambia na wenyeji Tanzania.

No comments:

Post a Comment