10 October 2011

JKT Ruvu yainyuka Mtibwa 3-2

Na Speciroza Joseph
TIMU ya JKT Ruvu jana, imeibuka na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Mtibwa Sugar ya Morogoro katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliopigwa Uwanja wa Chamazi, nje ya
jiji la Dar es Salaam.
Kwa ushindi huo, JKT imepanda mpaka nafasi ya tatu kwa pointi 15, sawa na Azam FC na Mtibwa ila zinatofautiana kwa mabao.

Katika mchezo huo, Mtibwa ndiyo ilianza kufunga bao dakika ya tisa lililofungwa na Vicent Barnabas, kwa shuti la mbali akiunganisha krosi ya Issa Rashid.Kufungwa kwa bao hilo kuliiamsha JKT, ambapo dakika ya 27 timu hiyo ililiandama lango la Mtibwa na kupata kona iliyopigwa na Hassan Kikutwa, ambayo ilitinga moja kwa moja wavuni na kumuacha kipa Deo Munishi, akikosa la kufanya.

JKT iliendelea kuliandama lango la Mtibwa na dakika ya 36, Rajab Chau aliifungia bao la pili timu yake akiunganisha mpira wa adhabu uliopigwa na Emmanuel Linjechele na kufanya maafande hao, kuongoza katika dakika 45 za kwanza.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi ambapo Mtibwa, ilionekana ikitaka kusawazisha ambapo kama washambuliaji wake wangekuwa makini wangepata bao.Nafasi ambazo watajutia Mtibwa ni zile za dakika za 49 na 68 ambapo Ally Mohamed na Said Rashid, kama wangekuwa makini wangeifungia timu yao mabao kwani mashuti waliyopiga yalitoka nje na mengine kudakwa na kipa.

Pamoja na kuandamwa na mashambulizi, JKT ilitulia na kufunga bao la tatu dakika ya 85 lililofungwa na Stanley Nkomola kwa mkwaju wa penalti, baada ya beki Salvatory Ntebe kumwangusha Hussein Bunu ndani ya eneo la hatari.

Mashabiki wa JKT wakianza kuinuka vitini dakika za ziada, ndipo beki Ntebe aliifungia Mtibwa bao la pili akisawazisha makosa yake kwa shuti jepesi na kufanya dakika 90 zikimalizika JKT kuibuka na ushindi wa mabao 3-2.

No comments:

Post a Comment