10 October 2011

Mashindano ya Muungano yafutwa

Na Mwandishi Wetu
MICHUANO ya netiboli ya muungano mwaka huu, imefutwa kutokana na Chama cha Netiboli Zanzibar (CHANEZA), kukabiliwa na Uchaguzi Mkuu.CHANEZA imekiandikia
 barua Chama Cha Netiboli Tanzania Bara (CHANETA), kukitaka kusitisha maandalizi ya michuano hiyo kwa kuwa wanakabiliwa na Mkutano Mkuu utakaombatana na uchaguzi.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Kaimu Katibu Mkuu wa CHANETA Rose Mkisi, alisema sababu iliyotolewa na CHANEZA ni ya msingi hivyo wanaungana nao kwa hatua hiyo.

Alisema kutokana na hali hiyo CHANETA, imeamua kuandaa mashindano ya kuadhimisha miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara kwa kufanya mashindano yatakayohusisha timu 10 za netiboli.
Rose alisema mashindano hayo, yataanza kutimua vumbi Novemba 30 hadi Desemba 9, mwaka huu ambapo mahali yatakapofanyika patatangazwa mapema mwezi huu.

Alizitaja timu nane za Tanzania Bara, zitakazoshiriki michuano hiyo kuwa ni JKT Mbweni, Filbert Bayi, Jeshi Stars, Magereza, Polisi Dar es Salaam, Polisi Mbeya na Hamambe Mbeya.
Alisema wameiomba CHANEZA, kutoa timu mbili kushiriki ili kusherehekea miaka hiyo 50 ya Uhuru na mafanikio ya CHANETA tangu kuanzishwa kwake mwaka 1971.

No comments:

Post a Comment