Na Frank Balile
TIMU za soka za Simba na Ruvu Shooting, zimeingiza sh. milioni 14.755,000, katika mechi yao ya Ligi Kuu Bara iliyochezwa kwenye
Uwanja wa Azam Chamazi, Dar es Salaam, juzi.
Akizungumza jana mjini Dar es Salaam, Msemaji wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Boniface Wambura, alisema fedha hizo zimetokana na viingilio vya mashabiki uwanjani hapo.
Wambura alisema kuwa, watazamaji waliokata tiketi kushuhudia mechi hiyo walikuwa 2,794, ambapo kiingilio kilikuwa sh. 5,000 kwa mzunguko na sh. 10,000 kwa VIP.
Alisema mashabiki waliokata tiketi za VIP walikuwa 157.
Msemaji huyo alisema baada ya kuondoa gharama za mchezo na Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ambayo ni sh. 4,180,763, kila timu ilipata sh. 3,172,271.19.
Alisema mgawo mwingine ulikwenda kwa uwanja ambao ni sh. 1,057,423.70, TFF walipata sh. 1,057,423.70 na Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 528,711.86.
Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA walipata sh. 422,969.49 na Baraza la Michezo la Taifa (BMT) ni sh. 105,742.37.
Wakati huo huo, Wambura alisema mdhamini wa Ligi Kuu ya Vodacom, kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom, tayari imetoa hundi ya nauli kwa timu ambazo zinashiriki ligi hiyo.
Ofisa huyo alisema mgawo uliotolewa ni kwa ajili ya Septemba na Oktoba.
Alisema tayari klabu husika zimeanza kuchukua hundi zao kutoka TFF, ambapo kwa Septemba kila klabu imepata sh. 4,732,142, wakati Oktoba ni sh. 5,622,321.
Wambura alisema kuwa, kwa miezi hiyo miwili, hivyo kila klabu imepata sh. 10,354,463.
No comments:
Post a Comment