21 October 2011

Makocha 30 kunolewa Novemba

Na Zahoro Mlanzi

SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limeteua makocha 30 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar kwa ajili ya kozi ya kupata
leseni C, itakayofanyika kuanzia Novemba 7 hadi 20, mwaka huu Dar es Salaam.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura alisema makocha hao wanatoka katika timu mbalimbali zikiwemo za Ligi Kuu Bara, Zanzibar, Daraja la Kwanza na ligi zingine.

Alisema kozi hiyo itasimamiwa na Wakufunzi wanne ambao ni Jan Poulsen, ambaye anatambulika na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), Sunday Kayuni na Kasimao Malogo kutoka Nigeria ambao wanatambuliwa na CAF na Kim Poulsen, ambaye ni kocha wa timu za vijana.

"Kozi hii inafanyika kwa mara ya kwanza nchini, ambayo itasaidia kupata makocha wa madaraja mengine kama B na kuendelea ambayo itasaidia kunoa viwango vya makocha wazawa," alisema Wambura.

Katika hatua nyingine, Wambura alisema wameandaa mpango wa maendeleo ya soka nchini, ambapo wanatoa fursa kwa wadau wote wa soka kuwasilisha mawazo yao kuhakikisha mchezo huo, unapiga hatua.

Alisema wanakaribisha maoni mbalimbali kupitia mtandao wao au kwa anuani ya TFF, na mwisho wa kuwasilisha ni mwishoni mwa mwezi ujao.

Wambura alisema maoni hayo yatakusanywa na Kurugenzi ya Ufundi ya TFF, ambapo baada ya kuyapitia watayawasilisha kwa Kamati ya Utendaji itayaandaa kwa ajili ya kupitishwa katika Mkutano Mkuu.

No comments:

Post a Comment