20 October 2011

Lowassa ang'aka

*Akana kumhujumu rais, kuchochea UV-CCM
*Akwepa kuongelea Dowans, kujivua gamba
*Asisitiza hajakutana na JK barabarani


Na Waandishi Wetu, Arusha

ALIYEKUWA Waziri Mkuu, Bw. Edward Lowassa amejitenga na tuhuma zilizogaa kuwa anaandaa mikakati ya kumhujumu
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete, akisema atakuwa mtu wa mwisho kufikiria au kupanga njama hizo.

Akizungumza na wandishi wa habari nyumbani kwake Monduli, Arusha jana, Bw. Lowassa alisema kuwa amemuunga mkono Rais Kikwete kwa dhati kwa muda mrefu na kushirikiana naye katika harakati nyingi za kifikra na za kiuongozi katika ngazi mbalimbali kwa miaka mingi.

Uamuzi wake kukutana wandishi wa habari jana, alisema hauna makusudi ya kuzozana na vyombo vya habari wala kwenda kinyume na utamaduni wa kimaadili wa chama chake, bali kutoa ufafanuzi na angalizo kwa pande hizo mbili ambazo zinaguswa na matukio yanayoendelea kutokea.

Bw. Lowassa ambaye alikataa katakata kuzungumzia masuala yanayoendelea kuvuma kwa sasa, ya Richmond, Dowans wala falsafa ya kujivua gamba ndani ya CCM, akiahidi kuyazungumzia wakati mwingine, alisema kumhusisha na tuhuma za kumhujumu rais ni mambo ya kipuuzi, kizushi na yenye malengo machafu.

Akifafanua tuhuma hizo zilivyo, Bw. Lowassa alisema wahusika wanavitumia vyombo vya habari na wamefikia hatua ya kudai kwamba ameanza kuandaa orodha ya kile wanachokiita madhambi ya Rais Kikwete, ambayo amepanga kuyasoma wakati wa kikao kijacho cha Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM.

"Ninaamini kwa dhati kabisa kwamba, waandishi wa habari wanaofuatilia kwa karibu na kwa umakini mwenendo wa masuala ya kisaiasa nchini wanatambua kwamba, watu wanaopenyeza taarifa hizi katika vyombo vya habari wanafanya hivyo kwa malengo ya kufikirika na kujisafishia njia kisiasa.

"Ni jambo lisiloingia akilini kunihusisha na kile kinachoitwa mikakati ya kumhujumu rais au chama ambacho mimi ni kada wake wa muda mrefu, mbunge anayetokana na chama hicho hicho na mtu anayeiongoza Kamati nyeti ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama na zaidi ya yote kiongozi wa ngazi mbalimbali za kisiasa na kiserikali nilizowahi kushikilia.

"Kuhusu hili, napenda kusema kwa uwazi kwamba, mbali ya ukweli kuwa sijapata kufikiria hata mara moja kuhusu hicho wanachokiita mabaya au madhambi ya rais, sina, wala siijui hiyo wanayoitaja kuwa ni orodha ya mabaya ya namna yoyote dhidi ya Rais Kikwete.

"Mbali ya ukweli kwamba huo ni uongo wa wazi, silika yangu kama mwanasiasa na mtu mwenye dhamana kubwa kwa watu wa Monduli na kwa taifa langu, haiwezi kamwe kunituma nianze kupanga mikakati ya kumhujumu kiongozi wetu mkuu au chama ambacho kimenilea na mimi mwenyewe nikakitumikia kwa uadilifu na kwa juhudi kubwa pengine kuliko ilivyo kwa hao wazushi.

Bw. Lowassa alikwenda mbali hadi kuzungumzia urafiki kati yake na Rais Kikwete: "Nilipatana kulisema hili na leo nalirudia tena. Mimi na Rais Kikwete hatukukutana barabarani."

Aliongeza: "Tangu serikali ya awamu ya nne iingie madarakani kuna kundi la watu limekuwa likifanya juhudi kubwa kunigombanisha na rais wakitumia kila aina ya hoja za kupikwa. Kundi hilo ... ndilo ambalo mwaka juzi lilipenyeza ndani ya chama chetu na katika jamii hoja kwamba nilikuwa nimejipanga kugombea urais kwa tiketi ya chama chetu katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana," alisema Bw. Lowassa.

"Mwenyekiti wetu wa Taifa, Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete hawawezi kamwe kuamini, kushawishiwa na propaganda chafu zinazoendeshwa na kikundi kidogo cha wanasiasa hao.

Kuhusu matuko ya UVCCM

"Kama hiyo haitoshi, wanasiasa hao hao baada ya kulitumia jina langu kama ajenda yao ya uzushi wa kila  namna, sasa wameanza kunihusisha hata na matukio ya kisiasa kama yale yaliyotokea majuzi tu hapa Arusha.

"Ndugu wanahabari baada ya kukaa kimya kwa muda mrefu sasa, nimeamua kuanza kuchukua hatua mbalimbali za kisiasa na kisheria ambazo anamini zitatoa majibu sahihi dhidi ya wale wote walio nyuma ya ajenda hizi chafu, kwa lengo la kuweka kumbukumbu sawia ndani ya chama changu na kwa jamii nzima ya Watanzania ambao kwa muda mrefu wamelishwa mambo mengi ya kizushi na wakati mwingine ya hatari dhidi yangu.

Hatua kwa vyombo vya habari

"Tayari nimepanga kuanza kuwasiliana na kuwasilisha malalamiko yangu kwa mamlaka husika zinazosimamia mienendo ya kimaadili na weledi wa kitaaluma wa vyombo vya habari kama vile Msajili wa Magazeti na Baraza la Habari Tanzania.

Alisema kama hiyo haitoshi, baada ya kukaa kimya kwa muda mrefu ameanza kufikiria na kujipanga kuchukua hatua za kisheria dhidi ya waandishi wa habari na wahariri ambao kwa makusudi wameamua kutumia vibaya uhuru wa habari ambao serikali imeutoa.

Alisema kuwa anaamini wote wanakubaliana kuwa uhuru usio na nidhamu ni fujo.

Mbunge huyo, aliwataka viongozi wenye mawazo ya namna hiyo kutambua kwamba, muda adhimu wanaoutumia kubuni na kuzusha uongo kila kukicha mbali ya kuwavunjia heshima wao wenyewe unavidhalilisha vyombo vya dola ambavyo vinafanya kazi kubwa kuhakikisha hujuma za namna yoyote dhidi ya viongozi na taifa zinadhibitiwa.

Alisema kuwa akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama ya Bunge na mtu aliyepata kuwa Waziri Mkuu anatambua na kuiheshimu kwa dhati kazi hiyo kubwa inayofanywa kwa weledi mkubwa na taasisi mbalimbali za dola zenye wajibu wa kuhakikisha ulinzi na usalama wa viongozi na taifa kwa ujumla.

Uchumi, ajira kwa vijana

Akizungumzia hali ya uchumi, Bw. Lowassa alisema kuwa uchumi wa dunia upo taabani na Tanzania inakabiliwa na hali mbaya, kwani shilingi inazidi kuporomoka vibaya na mfumuko wa bei unazidi kuelekea kubaya zaidi.

Aliongeza kuwa kuna tatizo kubwa la ajira kwa vijana, na wengi wao wamekuwa wakiishi katika hali ngumu, jambo ambalo alilitafsiri kuwa ni sawa na kukali  bomu la muda na litasababisha kuvunjika kwa amani, hivyo akashauri kutafuta suluhu ya mambo hayo.

Katika mapendekezo yake, Bw. Lowassa alisema serikali ikope fedha ijenge viwanda ambavyo vitaweza kuajiri vijana wengi nchini.

9 comments:

  1. baba mzazi,mheshimiwa lowasa,naomba useme sasa kwa sababbu amani haitapatikana kwetu sisi unaotuongoza hadi hao mafisadi wenye uchu wa madaraka utakapowatia kofuli midomoni mwao.sema usiogope.sisi wananchi tuko nyuma yako na hatuogopi mageuzi,sema mzee.
    Toka wakuzushie ili ujiuzulu ,nchi imebadilika sana,na sasa karibu tunaangamia kwa shida ya uongozi bora.
    Ukikaa kimya zaidi tutakimbia vyama pinzani kwa uoga .hatuna imani na viongozi wetu wa sasa.
    Wanatupiga porojo tu na tumechoka.tunahitaji utendaji kama ule ukiwa waziri mkuu.ukisikika unakuja tu,viongozi wote wanaanza kuhaha.
    Wanajua hucheki.na kamwe usicheke maana wanatupeleka korongoni hawa.
    Heshima yako kiongozi wetu..

    ReplyDelete
  2. Ndugu Lowassa kwa mujibu wa maelezo yako tatizo si vyombo vya habari bali wale wanaokuchafua. Sasa mbona huwataji hayo wanaokuchafua ambao umesema wanapenyeza uchafu huo kupitia vyombo vya habari? Kwa nini unavishutumu vyombo vya habari na kutaka visiandike habari hizo? Kwa nini unataka kuminya uhuru wa vyombo vya habari kwa tuhuma na mashtaka yasiyo na maana? Kwa nini unataka kutenganisha mtu binafsi na madaraka yake? Ukiwa kiongozi sahau suala la maisha binafsi. Katika maisha binafsi ndiko tunapata uadilifu na usafi. Kutenganisha maisha binafsi ya kiongozi na uongozi ni dhana inayoendeleza uchafu na ukiukwaji wa maadili. Huu ndio msingi wa ufisadi na dhuluma.

    Maelezo yako yanatupa ukweli wa mamba pale unaposema, "Nitakuwa ni mtu wa mwisho kufikiria au kupanga kumhujumu mwenyekiti wetu." Kwa kauli hii ina maana kwamba umo katika orodha ya wale wanaotaka kumhujumu Kikwete ingawa wewe ni wa "mwisho". Basi twambie ni lini uliipanga oradha hiyo ya wanaotaka kumhujumu Kikwete na wewe kujiweka wa mwisho? Je unaweza kutuhabarisha ni kina nani wengine katika orodha hiyo unayojiweka mwisho? Je ni wakati gani wewe wa "mwisho" uko tayari kumhujumu Kikwete?
    Ukiwa waziri mkuu hayo matatizo unayotaja yalikuwepo na wewe uliyaongezea kasi. Hivi ni hasara kiasi gani taifa limeta kutokana upuuzi wako kuingia mkataba wa Richmond hadi Dowans na taifa kuendelea kukosa umeme? Hizi bilioni 111 unapaswa kuzilipa wewe. Shule za kata ulizisimamia kwa nguvu zote. Utawala bora uliivunja kwa kuingiza maslahi binafsi katika uongozi wa umma. Kumbuka ya Richmond ndugu Lowassa. Ajira za vijana na ugumu wa maisha yote yanakugusa. Wa kwanza kujisahihisha ni wewe kwa kujiuzulu.
    Hizo nchi unazozitolea mfano kama Nigeria, Malaysia, Singapore, India, Uingereza, Ufaransa na Ujerumani, vyombo vya habari katika nchi hizi vinaandika zaidi maisha binafsi ya viongozi. Na kwa kufanya hivi wameweza kusaidia kuwaondoa madarakani viongozi wasio waadilifu kama wewe. Angalia sakata la waziri wa ulinzi wa Uingereza na kujiuzulu kwake.

    Usitishie vyombo vya habari. Ondoa banzi katika jicho lako. Bora ungekaa kimya huna la maana ulilolisema.

    ReplyDelete
  3. mzeee wanasema kobe akiinama ujue anatunga sheria au kimya kingi kina mshindo lakini hapo kwako sijaona yote mawili kashfa ni nyingi juu yako lakini hakuna uliyojibu yenye mashiko kwenye jamii umejibu mambo yenu binafsi kwenye chama chenu hayo ilibidi ukayaongee huko huko kwenye chama chenu si tunataka tusikie kuhussu uhusika wako dowans rich man from monduli.... unahusika?????????????????????????????? usivitishe vyombo vya habari acha wafanye kazi yao...

    ReplyDelete
  4. Mh. Lowassa kuwa mkweli zaidi na utaje hao kina Sitta na Nape maana hao ndio wabaya wako wanaokusakama kila wakilala wakiamka LOWASSA AVUE GAMBA, MAPACHA WATATU WAONDOKE CCM N.K. N.K.
    Huyu kijana Nape ndiye anayekuchafua kwa kulipiza kisasi cha wakati uleeee!!! kama unakumbuka alipokosa Uenyekiti wa Vijana CCM akiamini wewe ndio ulisababisha ulipokuwa Waziri Mkuu. Mshone mdomo huyu Mmakonde japo tabia ya wamakonde ni kusema sema hovyo hovyo.

    ReplyDelete
  5. LOWASSA UNAMSIFIA KIKWETE WAKATI YEYE NDIYE AMESEMA WEWE NI GAMBA LAZIMA UONDOKE MBONA WEWE UNAKUWA MNAFAKI KAMA ULIZALIWA PWANI? WEWE NAPE ANAPITA ANATANGAZA GAMBA NI LOWASSA JANA UNAITISHA PRESS CONFERENCE KUTISHIA MEDIA SHAME ON YOU! UNATUELEZA MAMBO YA AIBU ATI HAMJAKUTA BARABARANI MLIKUTANA CHUMBANI, NANI AMEOA MWENZAKE SASA? AKILI KAMA YA NG'OMBE WEWE LOWASSA NI MWIZI NA JANA UMEJIMALIZA MWENYEWE!

    ReplyDelete
  6. LOWASSA ALIYEKUCHAFUA NI NYERERE HAO WENGINE UNAWASINGIZIA TU. KWANI CHAMA NI CCM TU. WEWE LOWASSA, AZIZ NA KIKWETE ACHIENI CHAMA CHETU MNAKIUA. KIONGOZI ANAYESHINDWA KULINDA RASILIMALI YA TAIFA HAFAI. MNASHINDWA HATA KUUA MBU BALI KUTOROSHA MALI GHAFI KWENDA NJE NDIO MNAONA TIJA. WASWAHILI WANASEMA HUWEZI KUTENGANISHA MAJI NA TOPE. CCM JUU1

    ReplyDelete
  7. ndo maana nimesema bado tutaona mengi na kusikia; bora mmasai angekaa kimya badala ya kupandisha mori ambao hautulizi mtu!inatisha.angekaa kimya watu wangesahau hata ya dowans na babake richmond!

    ReplyDelete
  8. Mzee acha 'longo-longo' bado unayo kazi kubwa ya kuwashawishi wapiga kura kuhusu jitihada zako za kujisafishia njia ya kuingia Ikulu 2015.

    ReplyDelete
  9. Lowasa tunakukumbuka sana kwa mkwara wako hasa pale ulipokuwa unakalia matofali wakati wa kusimamia ujenzi wa Sekondari za Kata; lakini hili la Dowans na Richmond limekung'ang'ania. Pengine ukapate kikombe kwa Babu ili kupungunza jazba za Watanganyika lakini kutishia vyombo vya habari ni sawa na kumwagia Petroli kwenye nyumba ambayo tayari inaungua.

    ReplyDelete