19 October 2011

Kujiuzulu Lowassa kulinishtua-Sitta

*Asema alimbabatiza bila kutarajia hali hiyo
*Akiri kushindwa kuahirisha kikao cha bunge
*Asema mpambano dhidi ya Dowans bado mbichi


Na Edmund Mihale

WAZIRI wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Samuel Sitta, amesema kuwa
katika uongozi wake wa Spika wa Bunge la Tisa jambo lilomuumiza zaidi na kumshtua ni siku ambayo Bw. Edward Lowassa alipojiuzulu Uwaziri Mkuu.

Bw. Lowassa ambaye alikuwa Waziri Mkuu wa nane wa Tanzania alijiuzulu Februari 7, 2008 baada ya kutajwa katika ripoti ya Kamati ya Bunge iliyoongozwa na Mbunge wa Kyela, Dkt. Harrison mwakyembe kuchunguza kashfa ya utoaji zabuni bila kufuata taratibu kwa Kampuni ya kufua umeme wa dharura ya Richmond.

Katika taarifa hiyo, Bw. Lowassa aliyekuwa kiongozi wa shughuli za serikali bungeni, alitajwa kuwa alikuwa anashinikiza kampuni hiyo kupewa zabuni na hivyo kutakiwa apime mwenyewe maamuzi yake yameathiri vipi serikali na hadhi ya bunge, hivyo akaamua kujiuzulu kwa maelezo kuwa alikuwa anawajibika.

Akizungumza katika kipindi cha Dakika 45 kinachorushwa na ITV juzi usiku, Bw. Sitta alisema kuwa siku hiyo ilikuwa ngumu kwake kutoka na uamuzi uliochukuliwa na Bw. Lowassa, kwa kuwa hakuwa anautarajia.

"Baada ya ripoti ya Kamati Teule ya Bunge kuchunguza kashfa ya Richmond, nilitegemea kuwa wabunge watajadili, waoneshe upungufu na wapi ripoti hiyo imekosewa na tuijadili na kuifanyia kazi.

"Baada ya Dkt. Mwakyembe kumaliza kusoma hotuba hiyo kulikuwa na wabunge kama watano au sita hivi waliomba kuchangia taarifa hiyo lakini, Bw. Lowassa aliomba aanze kuchangia yeye kabla ya wabunge hao.

"Unajua kwa taratibu zetu, Waziri Mkuu ambaye ndiye kiongozi wa shughuli za serikali bungeni  anapoomba nafasi ya kuchangia lazima umpe kipaumbele, nilidhani anataka kurekebisha au kuchangia taarifa hiyo kumbe akatangaza kujiuzulu Uwaziri Mkuu.

"Waziri Mkuu anapojiuzulu maana yake serikali nayo imeanguka, hivyo hakukuwa na serikali, bunge likashindwa kuendelea na sikuweza kufunga bunge siku hiyo, ilinilazimu kumuona rais ili atoe maelekezo naye alifanya hivyo, nikaaihirisha bunge," alisema Bw. Sitta.

Alisema kuwa jambo hilo lilitokea huku akiwa hana matarajio, hivyo kumpa wakati mgumu kufanya uamuzi wa haraka.

Malipo ya Dowans

Bw. Sitta katika mahojiano hayo alisisitiza msimamo wake kutaka Dowans isilipwe mabilioni hayo, akisema kuwa msimamo wake upo pale pale na kwamba atapambana hadi mwisho.

“Unajua kuwa ukifika katika umri wangu unakuwa umepitia na kuona mambo mengi, unatakiwa kuwa mkweli.

"Sikiliza, mbona mnakuwa kama hamna uzalendo, Dowans ni biashara ya kipumbavu…nawashangaa hata hao wanaotulaumu sisi kuwa ndio tumeifikisha nchi katika hatua hiyo ya kutakiwa kulipa deni hilo. Dowans ni wizi ambao kila Mtanzania anapaswa kuulaani ushenzi huu badala ya kushangilia,” alisema Bw. Sitta

Alifafanua kuwa mkataba ulioingia na kampuni hiyo haukuwa sahihi kwakuwa ulikiuka sheria za ununuzi.

Kwa mujibu wa Bw. Sitta, kampuni hiyo ilitakiwa kuingia mkataba na Bodi ya Wakurugenzi ya TANESCO lakini zabuni hiyo ilipitiwa na tume iliyoundwa kutoa serikalini, jambo ambalo lilikuwa ni ukiukaji wa mkataba huo.

Alisema kuwa bodi ya TANESCO ilindaa mkataba kwa kuipa kampuni hiyo vipengele 24 ambayo ilitakiwa kuvitimiza ndipo ipewe zabuni hiyo, lakini tume ilivipunguza hadi kufikia vinne ambavyo navyo ilishindwa kuvitimiza.

Alisema kuwa tume hiyo iliipa kampuni hiyo mkataba wa mwaka mmoja lakini waziri aliyejiuzulu (hakumtaja jina) aliongeza mkataba huo na kuwa wa miezi 24.

Ingawa Bw. Sitta hakutaja jina waziri huyo, mawaziri wawili waliojiuzulu kwa kashfa hiyo zaidi ya Bw. Lowassa, ni wawili, Bw. Nazir Karamagi na Dkt. Ibrahim Msabaha, waliokuwa wameshika wizara ya Nishati na Madini kwa nyakati tofauti.

Bw. Sitta ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Urambo Mashariki, alisema kampuni hiyo baada ya kufikisha miezi 22 ikiwa imelipwa fedha za capacity charge ( za kuweka mitambo) sh. milioni 152 kila siku bila kuzalisha umeme iliuzwa kwa kampuni ya Dowans

"Fedha hizi zilitosha kabisa kwa kampuni hiyo kujiendesha na baada ya kuuzwa ingekuwa na faida kubwa," alisema Bw. Sitta.

Alisema ni jambo ambalo halimuingii akilini kuona kuna watu wanajiita Mahakama ya Usuluhishi, wanakaa katika Hoteli ya MovenPick jijini Dar es Salaam na kuamua kuwa serikali iilipe Dowans mabilioni ya shilingi huku wakiwa wamelipwa fedha za kukaa katika hoteli hiyo kuamua mambo yasiyofaa.

Bw. Sitta alifananisha mkataba huo sawa na mwizi wa simu ambaye alitaka kuiuza kwa sh. 100,000 akalipwa malipo ya awali ya sh. 60,000 lakini aliyenunua akataa kumalizia malipo yaliyobaki, huku akihoji, "je, mwizi huyo atakuwa na haki ya kudai malipo hayo wakati akijua kuwa simu hiyo ni mali ya wizi?"

Bw. Sitta, maarufu kama Spika wa Kasi na Viwango, katika Bunge lililopita alisimama imara pamoja na baadhi ya wabunge waliojipambanua kama wapambanaji wa ufisadi kupinga Kampuni ya Richmond (na baadaye Dowans) na kuishinikiza serikali ivunje mkataba huo.

Alisema kuwa Watanzania wanapaswa kuwa na uzalendo wa kulipigania taifa lao badala ya kukatishwa tamaa kwa kutishwa kuwa Dowans lazima ilipwe.

“Kwanza nikuhakikishie huu si mwisho wa mapambano, Dowans kulipwa ni sawa na kuhalalisha ushenzi wa majizi hayo, hatuwezi kushangilia, nitapinga hadi mwisho," alisema Bw. Sitta.

ICC iliitia hatiani TANESCO kwa kosa la kuvunja mkataba na Dowans iliyokuwa ikitetewa na wakili wa kimataifa, Bw. Kennedy Fungamtama na ikaiamuru iilipe tuzo hiyo ya sh bilioni 94 na riba ya asilimia 7.5.

Hatua hiyo ya kuchelewesha malipo ya tuzo hiyo itaifanya TANESCO sasa kulipa kiasi kikubwa zaidi, kwani riba imekuwa inaongezeka, na hadi tuzo hiyo inasajili na Mahakama Kuu nchini, Dowans ilikuwa inastahili kulipwa na Tanesco sh bilioni 113 badala ya sh bilioni 94.
 

6 comments:

  1. Mzee sitta nakunga mkono inabidi tusiangalie vyama vyetu vya siasa tuangalie taifa letu linakwenda wapi tumesha choshwa kuibiwa na wajinga wachache ambao wanatumia hadi vyombo vya dola kuhalalisha unjinga wao. Ila wakati umefika sasa tuungane wote watanzania tusijali chama au dini wala ukabila tusimame pamoja kupinga malipo ya dowans maana tunadhalilika sana tunapo kuwa nchi za wenzetu kuona tuna wasomi wengi sana wanasheria ila tuna shindwa kutetea maslai ya taifa letu. Sasa itakuwa nini maana ya kusoma nakuanzisha mavyuo mengi nchini halafu wasomi wenyewe hatuoni matunda yao. Ila tunaona uchafu wa wajinga wacheche ila nadhani Mungu yupo muda utafika tu yuko wapi gadaffi, Sadam, Mubarrak etc. Mzee Sitta tupo pamoja unanguvu kubwa sana ya umma inakusapoti

    ReplyDelete
  2. Kila mtanzania bila kujali chama cha siasa, kabila lake na wala dini yake chonde chonde amuakeni kuwaondoa washenzi wanaotaka kutuibia na sisi tunaona wakitumia makalatasi. Lengo lao ni moja tu wamuingize Lowasa Ikulu. Wakishahalalisha malipo ya Dowans watakuwa wametuambia mkataba wa Richmond haukuwa umekosewa bali ili kuwa ni siasa tu. Sisi tujuavyo mkataba ule ulikuwa wa kifisadi na wanasheria toka Tanesco na serikalini wamelipwa fedha nyingi sana ili waisaliti nchi yetu. Wanatufanya sisi mazezeta. Karamagi na kundi lake la mafisadi tuwaambie sasa inatosha. Tupo tayari kwenda mitaani watanzania wote tukatae wizi huu. Kwani tunajua wazi timu itakayofaidika na wizi huu. Na wamejitoa kabisa kwa lolote mladi wafaidike na wizi huu. Wala hakuna cha kitu kuitwa uwekezaji. Sitta na wenzako mlio wazalendo Mungu atawalinda na hila za mafisadi ambao wamedhamiria kutumaliza watanzania. Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Africa

    ReplyDelete
  3. Mzee Sitta tunakuunga mkono, Asante sana na Mungu Akubariki.

    ReplyDelete
  4. Lowassa katoka kuongea na taarifa yake kwa vyombo vya habari tumeisoma. Nami nina haya ya kusema:
    Ndugu Lowassa kwa mujibu wa maelezo yako tatizo si vyombo vya habari bali wale wanaokuchafua. Sasa mbona huwataji hayo wanaokuchafua ambao umesema wanapenyeza uchafu huo kupitia vyombo vya habari? Kwa nini unavishutumu vyombo vya habari na kutaka visiandike habari hizo? Kwa nini unataka kuminya uhuru wa vyombo vya habari kwa tuhuma na mashtaka yasiyo na maana? Kwa nini unataka kutenganisha mtu binafsi na madaraka yake? Ukiwa kiongozi sahau suala la maisha binafsi. Katika maisha binafsi ndiko tunapata uadilifu na usafi. Kutenganisha maisha binafsi ya kiongozi na uongozi ni dhana inayoendeleza uchafu na ukiukwaji wa maadili. Huu ndio msingi wa ufisadi na dhuluma.

    Maelezo yako yanatupa ukweli wa mamba pale unaposema, "Nitakuwa ni mtu wa mwisho kufikiria au kupanga kumhujumu mwenyekiti wetu." Kwa kauli hii ina maana kwamba umo katika orodha ya wale wanaotaka kumhujumu Kikwete ingawa wewe ni wa "mwisho". Basi twambie ni lini uliipanga oradha hiyo ya wanaotaka kumhujumu Kikwete na wewe kujiweka wa mwisho? Je unaweza kutuhabarisha ni kina nani wengine katika orodha hiyo unayojiweka mwisho? Je ni wakati gani wewe wa "mwisho" uko tayari kumhujumu Kikwete?
    Ukiwa waziri mkuu hayo matatizo unayotaja yalikuwepo na wewe uliyaongezea kasi. Hivi ni hasara kiasi gani taifa limeta kutokana upuuzi wako kuingia mkataba wa Richmond hadi Dowans na taifa kuendelea kukosa umeme? Hizi bilioni 111 unapaswa kuzilipa wewe. Shule za kata ulizisimamia kwa nguvu zote. Utawala bora uliivunja kwa kuingiza maslahi binafsi katika uongozi wa umma. Kumbuka ya Richmond ndugu Lowassa. Ajira za vijana na ugumu wa maisha yote yanakugusa. Wa kwanza kujisahihisha ni wewe kwa kujiuzulu.
    Hizo nchi unazozitolea mfano kama Nigeria, Malaysia, Singapore, India, Uingereza, Ufaransa na Ujerumani, vyombo vya habari katika nchi hizi vinaandika zaidi maisha binafsi ya viongozi. Na kwa kufanya hivi wameweza kusaidia kuwaondoa madarakani viongozi wasio waadilifu kama wewe. Angalia sakata la waziri wa ulinzi wa Uingereza na kujiuzulu kwake.

    Usitishie vyombo vya habari. Ondoa banzi katika jicho lako. Bora ungekaa kimya huna la maana ulilolisema.

    ReplyDelete
  5. Hata janja yako yakuanza kwaita waandishi wa habari kwako monduli wewe kama nani?? hu ni ujambazi tu wa kutumia hela zako ubisha usibishe umewalipa waandishi wote waliokuja monduli wewe ni nani?? Tumeshakujua vizuri wala usipoteze hela zako kudhani utarudia umaarufu labda uende nchii ingine sio tanzania. Lowasa si upumzike uliweka nadhiri kutawala?? ni wewwe tu Nchi hii Watu walio karibu yako hawakwambi ukweli unavyosemwa mitaani ???usijisumbue Tunakinai tukiona jina lako gazetini, pumzika na mkeo na wanao

    ReplyDelete
  6. Lowassa anaulizwa: Utajiri huu mkubwa kaupata wapi? Mbona king'ang'anizi hujaona watanzania wakisikia jina lako wanapata hasira na hata kinyaa! Pumzika kama Karamagi, furahia utajiri wako na tuachie tuendelee mbele. Unajishikiza na makanisa ukitaka wakutetee na kukusafisha.

    ReplyDelete