05 October 2011
Wananchi wanaafiki kuvuana magamba-Nape
Na Reuben Kagaruki
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema ushindi waliopata katika uchaguzi mdogo wa ubunge
Jimbo la Igunga na kwenye kata 17 za udiwani kielelezo kuwa wananchi wanakubaliana na mageuzi yanayofanyika ndani ya chama hicho.
Kauli hiyo ilitolewa Dar es Salaam jana na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Itikadi na Uenezi, Bw. Nape Mnauye wakati akizungumza na waandishi wa habari kutoa salamu kwa wananchi waliochagua chama hicho.
"Ushindi huu ni uthibitisho wa mageuzi tunayofanya ndani ya chama na kielelezo kuwa yanaugwa mkono na wananchi," alisema Bw. Nnauye huku akijivunia 'kampeni za kistaarabu' ambazo alidai chama hicho kiliendesha.
Akifafanua baadaye, alisema mafanikio hayo yamewapa hamasa zaidi ya kuendeleza falsafa yake ya kuvuana magamba, kwa maana ya kusimamia maadili zaidi, uwajibikaji zaidi na kuongeza fursa kwa vijana, lakini haina maana ya kufukuzana kwenye chama.
Mageuzi yanayofanyika ndani ya chama hicho ni ya wanachama wanaotuhumiwa kwa ufisadi kujivua gamba kwa kuachia ngazi za uongozi na hata uanachama. Kujiuzulu kwa aliyekuwa mbunge wa Igunga, Bw. Rostam Aziz na kuachia wazi nafasi hiyo kunahusishwa na kujivua gamba, ingawa yeye pamoja na sababu nyingine alisema amechoshwa na siasa uchwara ndani ya CCM na hakujivua gamba.
Aliendelea kutamba kuwa ushindi huo ni uthibitisho kuwa wananchi wamekataa siasa za fujo alizodai zilizokuwa zikiendeshwa na washindani wao wa karibu, CHADEMA, wakati wa kampeni za Igunga.
Hata hivyo, chama hicho mara nyingine kimekanusha tuhuma hizo na kutuma lawama kwa CCM kuwa ndio walikuwa wameandaa vijana katika katika makambi yao ili kufanya fujo.
"Watu kujitokeza kidogo kupiga kura ni moja ya sababu za ubakaji wa demokrasia uliofanywa na CHADEMA," alisema Bw. Nape, katika kinachoonekana ni majibu ya tuhuma zilizotolewa na CHADEMA kuwa CCM kimekuwa kinanunua shahada za kupigia kura ili kuwazuia watu wenye mwelekeo wa kukipinga kujitokeza kupiga kura.
Kutokana na matokeo hayo CCM Mkoa wa Dar es Salaam imeandaa mapokezi makubwa ya timu ya kampeni iliyokuwa Igunga yatakayofanyika Oktoba 8, mwaka huu ambayo utafuatia na mkutano.
Alisema timu hiyo ya kampeni ilianza kuondoka Igunga jana ambapo itapiga kambi mkoani Singida kujumuika na wananchi kusherekea ushindi wa diwani na baadaye itakuwa Dodoma na Oktoba 7 itakuwa mkoani Pwani kabla ya kupokewa jijini Dar es Salaam Oktoba 8, mwaka huu.
Akizungumzia hali ya kampeni katika Jimbo la Igunga, Bw. Nape alisema ifike hatua watu waseme wanataka siasa za ustaarabu. Alisema siasa zilizokuwa zikiendeshwa na CHADEMA zilikuwa ni ubakaji wa demokrasia.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Huyo Nape ni mnafiki kama mwenyekiti wake na utakiua chama, coz hata siasa hujui ndugu yangu wewe, unashindwa kuelewa kwa nini watu hawakujitokeza kupiga kura? wewe wa ajabu sana
ReplyDelete