20 October 2011

Botswana kuzipiga bao Nigeria, Cameroon Chalenji

Na Zahoro Mlanzi

SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limesema Botswana ina nafasi nzuri ya kushiriki mashindano ya Kombe la
Afrika Mashariki na Kati (Chalenji), mwaka huu kutokana na ukarimu wake kwa nchi za ukanda huo.

Mashindano hayo yanatarajia kufanyika kwa mara ya pili mfululizo, Dar es Salam ambapo kwa mwaka huu yamepangwa kuanza kutimua vumbi Novemba 24, mwaka huu.

Akijibu swali la waandishi wa habari Dar es Salaam juzi kuhusu timu zilizoalikwa katika mashindano ya mwaka huu na maandalizi yake, Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura alisema kwa anavyojua kuna nchi zaidi ya nne zimeomba kushiriki.

"Kwa taarifa ya awali ambayo ilitolewa na CECAFA (Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati) zilitajwa ni nchi kama Nigeria, Cameroon, Zambia na Zimbabwe ambazo zimeomba kushiriki.

"Na baadaye ikajitokeza Botswana nayo ikiomba kushiriki katika mashindano hayo, hivyo Sekretarieti ya CECAFA itakuwa na kazi kubwa katika kuchagua timu zipi zishiriki," alisema.

Alisema timu zote hizo ni nzuri katika bara la Afrika, hivyo itakuwa ni changamoto kwa nchi za ukanda huo kushindana nazo.

Akiizungumzia Botswana, alisema anafikiri inaweza kupewa nafasi kutokana na uhusiano wao mzuri na CECAFA, kwani mashindano mengi yanayofanyika nje ya ukanda huo, nchi hiyo imekuwa ikitoa nafasi kwa nchi za CECAFA.

"Unajua Makao Makuu ya COSAFA (Baraza la soka kwa Nchi za Kusini mwa Afrika) yapo Gaborone na ndiyo maana Botswana hutoa nafasi kwa CECAFA kuchagua nchi iwakilishe ukanda huo, wakati ule wa michuano ya wanawake iliyofanyika Zimbabwe, Tanzania ilipeleka timu," alisema Wambura na kuongeza;

"Hivi karibuni pia timu yetu ya Vijana chini ya umri wa miaka 20 (Ngorongoro Heroes), imepata mwaliko kupitia CECAFA ikashiriki michuano ya vijana itakayofanyika Gaborone, Botswana," alisema.

Aliongeza kuwa CECAFA, imekuwa ikitoa nafasi kwa Tanzania kutokana na vipindi vyote hivyo, timu za hapa nyumbani ndizo zinazoonekana kuwa hai tofauti na nchi nyingine.

Kwa mujibu wa CEACAFA, wanahitaji zaidi ya sh. bilioni moja, ili kuandaa michuano hiyo nchini na tayari nchi 11 wanachama wamekumbushwa kuziandaa timu zao mapema.

Fedha hizo ni kwa ajili ya kugharamia tiketi za timu na viongozi, malazi, posho na chakula kwa siku zote za mashindano.

Timu ya taifa ya Tanzania Bara (Kilimanjaro Stars), ndiyo mabingwa watetezi wa mashindano hayo, baada ya kuifunga Ivory Coasta bao 1-0 katika fainali iliyopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment