*Yaichapa Ruvu 2-0
Na Speciroza Joseph
VINARA wa Ligi Kuu Bara, timu ya Simba imezidi kujikita kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo baada ya
kuifunga Ruvu Shooting ya Pwani mabao 2-0 katika mchezo uliopigwa Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam.
Kwa ushindi huo, Simba imefikisha pointi 24 ikiizidi JKT Oljoro ambayo ipo nafasi ya pili kwa pointi tano, Azam FC inafuata nafasi ya tatu kwa pointi 18 na Yanga ina pointi 15 kabla ya mchezo wa leo dhidi ya Toto African.
Katika mchezo huo wa jana, Ruvu ilianza kwa kuliandama lango la Simba katika dakika za sita na 10 ambapo kama wangekuwa makini wangefunga mabao ya mapema.
Safu ya ushambuliaji ya Ruvu iliongozwa na Abdallah Juma ambaye alikosa bao la wazi dakika ya sita kwa shuti lake kutoka nje ya goli.
Baada ya kushambuliwa sana, Simba ilitulia na kufanya shambulizi la nguvu dakika ya 25 kutokana na Uhuru Seleman kuichambua ngome ya Ruvu na kupiga shuti lililogonga mwamba na kurudi ndani na mabeki kuokoa.
Timu hizo ziliendelea kushambuliana kwa zamu ambapo Ruvu ilionekana kushambulia mara nyingi zaidi na mpaka dakika 45 zikimalizika timu hizo zilitoka suluhu.
Kipindi cha pili kilianza na Simba kufanya mabadiliko ambapo Uhuru alitoka na kuingia Haruna Moshi 'Boban' mabadiliko ambayo yalibadilisha mchezo kwa upande wa Simba.
Dakika tatu baada ya kipindi hicho kuanza, Emmanuel Okwi aliifungia Simba bao la kwanza ikiwa ni bao lake la tano katika ligi hiyo, kutokana na kazi nzuri iliyofanywa na Boban aliyeonana safi na Jerry Santo kabla ya kumpasia mfungaji.
Simba iliendelea kuliandama lango la Ruvu na dakika ya 54, Boban aliifungia timu yake bao la pili kwa shuti nje ya eneo la hatari na kumfanya kipa Benjamin Haule akiruka bila mafanikio.
Kufungwa kwa mabao hayo kuliifanya Simba izidi kutakata ambapo dakika ya 55, Patrick Mafisango alitoka na kuingia Shomari Kapombe na kuwafanya mashabiki wao kushangilia muda wote kutokana na timu yao kucheza vizuri.
Baada ya kuona inaelemewa, Ruvu iliamua kufanya mabadiliko ambapo iliwatoa Abdallah Juma na Raphael Kayela na nafasi zao kuchukuliwa na Seif Abdallah na Abdallah Abdaulrahman, lakini hata hivyo mabadiliko hayo hayakuzaa matunda.
Timu hizo ziliendelea kushambuliana kwa zamu na mpaka kipyenga cha mwisho kikipulizwa, Simba iliibuka na ushindi wa mabao 2-0.
Simba:Juma Kaseja, Nassor Said, Juma Jabu, Obadia Mungusa, Juma Nyosso, Santo, Mafisango/Kapombe, Ulimboka Mwakingwe/Frank Sekule, Okwi, Felix Sunzu na Uhuru/Boban.
Ruvu:Benjamin Haule, Michael Pius, Paul Ngalema, George Michael, Shaaban Suzan, Idd Nyambiso, Ayoub Kitala, Hassan Dilunga, Abdallah Juma/Abdallah Seif, Kassim Linde/Juma Mdindi na Keyala/Abdulrahim.
Ligi hiyo itaendelea tena leo kwa kupigwa mchezo kati ya mabingwa watetezi Yanga itakayokaribisha Toto ya jiji Mwanza, mchezo utakaopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment