24 October 2011

Arusha watamba mbio za baiskeli

Na Mwandishi Wetu, Mwanza

RICHARD Laizer wa Mkoa wa Arusha ameibuka bingwa wa mbio za wazi za baiskeli za Vodacom Mwanza Cycle Challenge, ambazo
zilianzia Shinyanga na kumalizikia Jijini Mwanza.

Bingwa huyo alipata ushindi huo kwa upande wa wanaume, katika mashindano yaliyoshirikisha wapanda baiskeli 400.

Baada ya kuibuka na ushindi huo, Laizer ambaye alitumia saa 5:02:28 kumaliza mbio hizo za kilometa 196, alikabidhiwa zawadi ya fedha sh. milioni 1.5, na kupewa taji lililokuwa likishikiliwa na Hamis Clement.

Mindi Mwagi wa Shinyanga, alikuwa wa pili baada ya kutumia saa 5:02:29 ambaye amezawadiwa sh. milioni moja, wa tatu alikuwa Said Jumanne wa Arusha aliyezawadiwa sh. 700,000 yeye akiuwakilisha mkoa wa Arusha.

Kwa upande wa wanawake kilometa 80, Mkoa wa Arusha uliibuka kidedea baada ya mshiriki wake, Sophia Hussein kuwabwaga washiriki wenzake zaidi ya zaidi 60 baada ya kutumia saa 2:25:13 na kunyakua sh. milioni 1.1 na kuvikwa taji lililokuwa likishikiliwa na Sophia Adison wa Arusha.

Mshindi wa pili katika mbio hizo alikuwa Mwajuma Mussa, pia wa Arusha aliyetumia saa 2:25:40 na kukabidhiwa sh. 800,000.

Nafasi ya tatu ilichukuliwa na Salome Donard wa Shinyanga na kunyakua sh. 600,000 ambapo alitumia saa 2:26:21.

Akizungumza mara baada ya mashindano hayo, Laizer alisema kilichomsadia ni mazoezi na maandalizi mazuri aliyoyapata, ingawa mlima wa Bugando wa ulimsumbua katika mashindano hayo.

Naye Mkurugenzi wa Vodacom Tanzania Kanda ya Ziwa, Steven Kingu ambaye alikuwa mgeni rasmi aliwapongeza washiriki wote hususani washindi na kuahidi kwamba kampuni yake itaendelea kuratibu michuano hiyo, ili kuifanya ya kimataifa.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Masoko wa Kampuni ya Serengeti Breweries Limited (SBL), Ephraim Mafuru ambao ni wadhamini wenza kupitia kinywaji cha Malta Guinness, alisema hawajutii kudhamini michuano hiyo kutokana na hadhi iliyonayo.

No comments:

Post a Comment