02 September 2011

Yanga yashtukia janja ya TFF

*Yasema logo ya Vodacom imekwisha

Na Addolph Bruno

KLABU ya Yanga imesema imeshtukia mbinu za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF),  kuwakoroga, huku likiegemea kwenye logo ya
wadhamini wa Ligi Kuu ya Vaodacom ili wasilipe fedha wanazolidai  sh milioni 8.6.

Yanga inaidai TFF, pesa hiyo kati ya shilingi milioni 18.6 ambazo kati yake shilingi milioni 2.6 za kipa wao Yaw Berko alizozawadiwa mara baada ya kumalizika kwa michuano ya kombe la Kagame na zingine milioni 16 ni pesa za klabu hiyo za ushindi wa kutwaa kombe la hilo.

Akizungumza na waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa Yanga, Louis Sendeu, alisema klabu hiyo imeishtukia TFF kutumia mwanya huo, baada ya kuona vikwazo vingi vinatolewa katika suala la logo, ambalo tayari wamelimaza na Vodacom, huku wakijua kuwa,  wanawadai.

Yanga hivi karibuni imekataa kuvaa jezi zenye nembo (logo) ya rangi nyekundu kifuani,  zilizotolewa na mdhamini mkuu wa ligi hiyo, Kampuni ya simu za mkononi Vodacom, kwa madai kuwa, haiendani na katiba yao.

Sendeu alisema kimsingi mpaka leo, TFF haijampatia Berko fedha zake sh. milioni 2.6 na kuitaka imlipe mara moja kipa huyo bora wa msimu uliopita.

Pia, fedha nyingine sh. milioni 8,  za klabu, wanazolidai shirikisho hizo, wanataka zilipwe haraka.

Alisema baada ya kuona suala la fedha za Berko linakuwa gumu,  klabu iliamua kumpatia Berko fedha alizokuwa akilidai shirikisho hilo, ili atakapokabidhiwa na TFF, azirejeshe.

Alisema tayari TFF imeilipa Yanga sh. milioni 10 ,siku chache kabla ya mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya Simba, ambapo kati ya hizo, sh. milioni 8.6. bado hazijalipwa.

"Sisi tunaishangaa TFF,  tangu suala hili la logo (nembo) liibuke,  imekuwa ikijaribu kutuwekea mazingira magumu kupitia kauli zao, kwa mfano, awali walisema tukikataa, tutakosa sh. milioni 4, za kila baada ya miezi mitatu kwa ajili ya nauli na vifaa." 

"Haikuishia hapo, baada ya kuona msimamo wetu upo pale pale, ilidiriki kusema, tutakosa fedha za ubingwa wa Ligi Kuu Bara kama tutatwaa kombe, hii ni mbinu ambayo sisi tumeiona inafanyika ili tusipewe fedha zetu zilizobaki," alisema Sendeu.

Akizungumza kuhusu nembo ya Vodacom kwenye jezi, Katibu Mkuu, Celestine Mwesigwe,  amethibitisha klabu hiyo kukubaliana na kampuni ya Vodacom kutumia rangi nyeusi,  badala ya nyekundu ya awali.

Alisema Yanga waliamua kulifuatilia kwa makini suala hilo ili kuijengea mazingira mazuri klabu hiyo kwa siku za usoni, kwa sababu inaendeshwa na wanachama.

Akifafanua utaratibu uliotumika kulimaliza suala hilo, alisema Kampuni ya Vodacom ilifanya mazungumzo na Yanga kupitia Mwenyekiti wao, Llyod Nchunga, aliyetia saini kwenye mkataba mpya siku chache, baada ya Yanga kuiandikia barua TFF kuitaka jambo hilo limalizwe kisheria.

No comments:

Post a Comment