02 September 2011

Vodacom yawapa mbio za mashua milioni 8/-

Na Zahoro Mlanzi

KAMPUNI ya simu za mkononi ya Vodacom, imedhamini timu ya Taifa ya mbio za mashua kwenda Maputo kwa kutoa sh. milioni 8.Fedha hizo zitawapeleka washiriki
watatu mjini Maputo,  Msumbuji kushiriki mashindano michuano ya Afrika 'All Africa Games), itakayoanza leo na kumalizika Septemba 11, mwaka huu.

Wachezaji hao ni Mwambao  Helef, Halife Mpondi na Hassan Said, ambao wameondoka jana kwenda mjini Maputo.

Mashindano hayo yanajulikana kama All African Games Sailing na kwamba, timu hiyo ilianza kujifua kwenye ufukwe wa Yacht Club jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari Dar es Salaam, jana, ilieleza kwamba, Mwenyekiti wa Kamati ya Utendaji ya Chama cha Mashua Tanzania (TSA), Phillemon Nassari, alisema ana uhakika vijana wake ambao wamefanya mazoezi kwa kipindi cha miezi mitatu, wataliwakilisha vema taifa na kuliletea medali ya dhahabu.

Alisema mbio hizo zitakazoshirikisha mataifa mbalimbali ya Afrika, zitakuwa na changamoto kubwa baada ya kila nchi kudai kwamba, imejiandaa vizuri ili kuwa bingwa wa jumla kwa mashindano hayo.

"Fedha hizi zilizotolewa na Vodacom Tanzania, ni matumaini yetu zimetoa hamasa kwa washiriki wetu kwenda kufanya vizuri Msumbiji, wamejiandaa vizuri kwa muda wa miezi nane,  ambapo kila wiki walikuwa wakifanya mazoezi mara moja kwenye ufukwe wa Yatch Club," alisema Nassari.

Mbali na hayo, mwenyekiti huyo aliiomba serikali kuigeukia na kuitilia uzito michezo mingine, ikiwemo ya baharini, hususan wa mashua.

Naye, mchezaji Alli Bush ambaye ni bingwa wa mashua kwa Afrika, aliyekuwa akifanya mazoezi na wawakilishi hao, alisema vijana hao wameiva kwenda kuiwakilisha Tanzania kwenye michuano hiyo ya kimataifa.

Kwa upande wake, Ibrahim Kaude ambaye ni Ofisa Udhamini wa Vodacom Tanzania, alisema kampuni yake imekuwa ikidhamini michezo mbalimbali nchini, imeona ni vema kuwekeza katika mchezo huo wa mashua.

"Tunajisikia fahari kuwa mmoja wa wadau waliofanikisha kuisafirisha timu hiyo ya taifa na tunaendelea kudhamini michezo mingine, lengo likiwa kupandisha hadhi ya Tanzania katika tasnia ya michezo duniani," alisema Kaude.

Mwakani, Tanzania inatarajiwa kuwa mwenyeji wa mashindano ya mbio za mashua za All African Games Sailing, yatakayofanyika Agosti 4 hadi 14, kwenye ufukwe wa Msasani chini ya usimamizi wa Yatch Club.

No comments:

Post a Comment