02 September 2011

Mbunge kuongoza wananchi 'kuvamia, ofisi za DAWASCO

Na Willbroad Mathias

MBUNGE wa Jimbo la Ubungo,Dar es Salaam, kwa tiketi ya CHADEMA,Bw. John Mnyika, ametishia kuongoza wananchi wa Kata ya Goba kuandamana hadi
ofisi wa  Shirika la Maji afi na Maji Taka (DAWASCO) iwapo itafika kesho bila wananchi wake kupata huduma hiyo.

Amesema hatua hiyo inalenga kuunganisha nguvu ya umma ili kuhakikisha hatua za haraka za kuwapatia wananchi hao maji zinachukuliwa.

Taarifa ya mbunge huyo kwa vyombo vya habari ilieleza kuwa mbali na maandamano hayo atachukua hatua za ziada kwa kukutana na meya, mkurugenzi na uongozi wa manispaa hiyo ili kuweza kuchukua hatua za haraka kuhusu tuhuma zilizotolewa kuwa kamati ya maji Goba ‘imetafuna’sh. milioni 18 zilizotolewa Agosti 28, 2011.

Alisema hiyo ndiyo ilisababisha kulimbikizwa kwa deni la  DAWASCO. Alisema atahakikisha madeni maji yanalipwa  kwa wakati na huduma ya maji inarejeshwa kwa wananchi wa kata ya hiyo.

"Mara baada ya kuingia ofisini Agosti  29 na 30 mwaka huu nilifuatilia na kubaini kwamba maji yamekatwa kwenye Kata ya Goba kutokana na DAWASCO kudai kamati ya mradi wa maji sh. 18,108,478,"alisema Bw. Mnyika 

Alieleza , katika kufuatilia deni hilo alipata taarifa za Kamati ya Maji kuwasilisha malalamiko DAWASCO ya kutokukubaliana na kiwango hicho cha deni na pia kwa Manispaa ya Kinondoni kuhusu matatizo ya kiutendaji na kifedha katika mradi huo wa maji ikiwemo ya upotevu wa fedha.

Mbunge huyo alisema katika ufuatiliaji wake alibaini kwamba matatizo ya maji katika Kata ya Goba kama ilivyo katika kata nyingine katika Jimbo la Ubungo na Mkoa wa Dar es Salaam kwa ujumla yanatokana na matatizo ya kimfumo, kiuongozi, kifedha na kiutendaji yanayosababishwa na Kamati ya Mradi wa Maji Goba, DAWASCO, DAWASA, Halmashauri za Jiji na Wizara ya Maji.

Bw. Mnyika alisema ili kukabiliana na changamoto ya maji, mwishoni mwa  Januari mwaka huu aliitisha kongamano la maji katika Jimbo la Ubungo na kuzungumza na wananchi.

Alisema pamoja na kuwasilisha ripoti ya kongamano husika kwa DAWASCO, DAWASA, Manispaa ya Kinondoni na Wizara ya Maji, hatua muhimu kuhusu matatizo katika mradi wa maji Goba na maeneo mengine hazikuchuliwa kwa wakati.

"Ili kuweza kuzisukuma mamlaka husika kutimiza wajibu wake, Februari 27, mwaka huu  nilifanya mkutano na wananchi ambapo risala ya wananchi pamoja na ripoti ya ukaguzi wa mradi wa mradi wa maji Goba ya mwaka 2007 zilizosomwa,"alisema mbunge huyo.

Alisema kuwa taarifa hizo  zilieleza bayana matatizo yaliyokuwepo kwenye kamati ya maji pamoja na mradi kwa ujumla ikiwemo yaliyohusu upotevu wa fedha.

Alisema kuwa kupitia mkutano huo maazimio mbalimbali yalifikiwa, ikiwemo ya kuitishwa kwa mkutano wa watumiaji wa maji kwa ajili ya kuvunja kamati iliyokuwepo na kuunda kamati mpya.

2 comments:

  1. Siyo GOBA pekee, hao dawasco ni bora tu wakanyang'anywa hiyo dhamana ya kugawa maji DSM, KIMARA tumesahau kabisa kuwa nyumba zetu zimeunganishwa na huduma ya maji, maji hayatoki kabisa wakati bomba kuu limepita hapo hapo, hao ni wajasiliamari wa kuuza maji kwenye magari yao.

    ReplyDelete
  2. Hivi kumbe kuna mamlaka ya maji hapa Dar??
    Maana maji ya bakhresa yanajulikana kuliko hayo ya DAWASCO???
    Kwani nchi hii haina kiongozi anayeweza kuwajibika kwa masuala kama haya bila ya kufuatwa fuatwa matakoni??

    Iko siku!!!!!!!!!!!!!!!

    ReplyDelete