16 September 2011

Yanga yaona mwezi

*Yaichapa Lyon 2-1

Na Speciroza Joseph

MABINGWA wa soka Bara, Yanga, jana ilizinduka na kufanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-1, dhidi ya African Lyon, katika mechi iliyochezwa
kwenye Uwanja wa Azam Chamazi mjini Dar es Salaam.

Walikuwa African Lyon walioanza mchezo kwa kasi na kulifikia lango la Yanga dakika ya kwanza, lakini mpira uliopigwa uliokolewa na kuwa kona ambayo haikuzaa matunda.

Yanag walijibu mashambuliaji na kulifikia lango la Lyon dakika ya 10, lakini shuti kali la Davies Mwape liliokolewa na kipa Juma Abdu.

Mwape alipata nafasi nyingine nzuri dakika ya 16, lakini shuti lake kali lilitoka nje.

Yanga ikicheza kwa kujiamini ilifanikiwa kupata bao la kwanza dakika ya 35, lililofungwa na Mwape, baada ya kuunganisha mpira wa krosi uliopigwa na Shamte Ally.

Dakika saba baadaye, Lyon walisawazisha bao hilo kupitia kwa Hamis Shengo, kwa mpira wa adhabu uliokwenda moja kwa moja wavuni.

Makosa ya mabeki wa Yanga, kumchezea vibaya Seleman Kassim na mwamuzi Mathew Akrama wa Rukwa kuamuru upigwe mpira wa adhabu, ambao ulizaa bao.

Bao hilo liliifanya Yanga kuzidisha mashambulizi, dakika ya 47, Pius Kisambale alishindwa kuitumia vizuri nafasi aliyopata  kwa kupiga shuti kali lililookolewa na kipa  Abdul wa Lyon.

Dakika ya 52, Adam Kingwande alifanikiwa kulifikia lango la wapinzani wao, lakini shuti lake lilitua mikononi mwa kipa Berko wa Yanga.

Rashid Gumbo aliyeingia badala ya Kigi Makasi, dakika ya 63, aliwainua vitini mashabiki wa Yanga, baada ya kuifungia bao la pili timu yake kwa shuti kali lililomshinda kudaka kipa Abdul na mpira kujaa wavuni.

Keneth Asamoah bahati haikuwa yake, kwani dakika ya 84, akiwa amebaki na kipa wa Lyon, Abdul alishindwa kuukwamisha mpira wavuni.

Baada ya mchezo huo kumalizika, Kocha wa Lyon, Jumanne Chale alisema kupoteza mchezo huo, hakuwezi kuwakatisha tamaa, watahakikisha wanasahihisha makosa yao kabla ya mchezo utakaofuata.

"Vijana wangu walicheza vizuri, lakini bahati haikuwa yetu, tunaangalia mbele kwa sasa," alisema.

Kwa upande wa Kocha Mkuu wa Yanga, Sam Time, alikataa kuzungumza lolote kwa waandishi wa habari, aliishia kusema 'no comment'.

Yanga kwa matokeo hayo, imetoka mkiani na kutua katika nafasi ya nane, ikiwa sawa kwa pointi na Toto African, lakini ikizidiwa kwa uwiano wa mabao.


Lyon: Juma Abdul, Hamis Shengo, Razack Khalfan, Hamis Yusuph, Seleman Kassim, Shaaban Aboma, Aziz Sibo, Adam Kingwande, Sino Augustino, Houd Mayanja, Benedict Jacob/Semmy Kessy.

Yanga: Yaw Berko, Shadrack Nsajigwa, Bakari Mbegu, Chacha Marwa, Abou Ubwa, Juma Seif 'Kijiko'/Geofrey Bonny, Nurdin Bakari, Kigi Makasi, Pius Kisambale, Shamte Ally/Keneth Asamoah, Davies Mwape.

1 comment:

  1. Haya kipofu kaona mwezi na kocha kagoma kusema lolote,haya na msemaji mkuu wa timu anasemaje?.Ndio mmeshaanza ligi?,Mwambieni aseme tu asiogope.

    ReplyDelete