Na Zahoro Mlanzi
KAMATI ya Nidhamu na Usuluhishi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), imepanga kukutana Septemba 24, mwaka huu kwa ajili ya kusikiliza mashauri
matatu dhidi ya Mwenyekiti wa Klabu ya Simba, Ismail Aden Rage na Ofisa Habari wa Yanga, Louis Sendeu.
Viongozi hao watafikishwa mbele ya kamati hiyo, kutokana na kuyumbisha mchezo wa Ngao ya Jamii kwa nyakati tofauti, kitendo ambacho kinadaiwa kiliathiri uingiaji wa watu katika mchezo huo kutokana na kauli walizotoa.
Rage alidai kuna kiongozi TFF, anakwamisha mchezaji wao Gervais Kago, asisajiliwe kwa wakati na Sendeu yeye ana mashtaka mawili la kuyumbisha mchezo pamoja na kumtolea lugha, inayoonekana kumsababishia matatizo mwamuzi Alex Mahagi, katika maisha ya kila siku.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari Dar es Salaam jana na Ofisa Habari wa shirikisho hilo, Boniface Wambura alisema awali kamati hiyo chini ya Mwenyekiti, Alfred Tibaigana ilikuwa ikutane Agosti 29, mwaka huu kusikiliza malalamiko ya TFF dhidi ya viongozi hao, lakini kikao kiliahirishwa kutokana na Kamati kutotimiza akidi (column) kwa wajumbe wake.
Alisema shirikisho hilo, liliwasilisha shauri jipya dhidi ya Sendeu, kutokana na matamshi yake dhidi ya mwamuzi Mahagi aliyechezesha mechi kati ya Yanga na Ruvu Shooting iliyochezwa Septemba 10, mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kumalizika kwa sare ya bao 1-1.
Alisema Sendeu alimshutumu Mahagi kuwa alisababisha timu yake, ikose ushindi kwa kuwabeba wapinzani wao na anamfahamu Mahagi kuwa ni mwanachama wa Simba na kadi nyekundu aliyompa kiungo wa Yanga, Haruna Niyonzima haikuwa halali.
Katika hatua nyingine, Wambura alisema mechi ya Ligi Kuu Bara kati ya Simba na Polisi Dodoma iliyochezwa juzi Uwanja wa Azam Chamazi, Dar es Salaam imeingiza sh. 16,839,000.
Alisema watazamaji waliokata tiketi kushuhudia mechi hiyo walikuwa 2,257, ambapo kiingilio kilikuwa sh, 7,000 kwa mzunguko na sh. 20,000 kwa viti maalumu (VIP) na waliokata tiketi za sh. 20,000 walikuwa 80.
Alisema baada ya kuondoa gharama za mchezo na Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), ambayo ni sh. 2,568,661.02 kila timu ilipata sh. 3,546,671.90 na mgawo mwingine ulikwenda kwa uwanja sh. 1,162,893.
Wambura alisema TFF ilichukua sh. 1,162,893, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 581,446, Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 465,157 na Baraza la Michezo la Taifa (BMT) sh. 116,289.39.
No comments:
Post a Comment