16 September 2011

Saba wanusurika kufa baharini wakienda Pemba

Na Mwajuma Juma, Zanzibar

WATU saba wamenusurika kufa baada ya mashua waliokuwa wakisafiria kuzama katika maeneo ya bahari ya Kiwanda cha Mbolea Mkoani Tanga.Watu hao ambao
walikuwa wakitokea Tanga kuelekea Wete Pemba walipatwa na
ajali hiyo saa 12:00 za asubuhi jana.

Mashua hayo yanayojulikana kwa jina la Asaa Robo inamilikiwa na Bw.Mkubwa Omar, ilikuwa ikiendeshwa na nahodha Issa Sharif.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba Bw. Yahya Rashid Bugi, amethibitisha kuzama kwa mashua hiyo ambayo ilikuwa imebeba mizigo
mchanganyiko.

Alisema watu hao waliokolewa wakiwa salama na boti ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

Kamanda Bugi alisema chanzo cha kutokea kwa ajali hiyo ni kujaa kwa maji katika mashua hiyo baada ya kusadikiwa kugonga kitu kizito ambacho kilipelekea kutoboka na kuingiza maji.

Hata hivyo alisema baada ya kutokea hitilafu hiyo watu hao walipiga simu na JWTZ kufika katika eneo la tukio na kuwaokoa
wakiwa salama.

“Chombo kilianza kuzama kidogo kidogo na watu hao waliweza kuwasiliana na Jeshi hilo kuenda kuwaokoa,” alisema Kamanda Bugi.

Aliishukuru JWTZ kwa kufanya kazi nzuri na kuweza kufika katika eneo hilo kwa wakati na kuwaokoa watu hao.

“Watu hao wapo salama, na Jeshi Limefanya kazi kubwa sana kukimbilia na kuwai eneo la tukio na kuwaokoa,” alisema.

Tanzania bado ipo katika msiba mkubwa wa kufuatia ajali mbaya ya kuzama kwa meli ya  Spice Islander iliyoua watu zaidi ya 200 huku  619 wakisalimika.

No comments:

Post a Comment