Na Zahoro Mlanzi
Mechi ya Yanga na Ruvu Shooting ya Pwani, umeingiza sh. 23,388,000 kutokana na watazamaji 6,566 walioingia uwanjani.Mchezo huo ulipigwa juzi Uwanja wa
Taifa, Dar es Salaam ambapo timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari Dar es Salaam jana na Ofisa Habari wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Boniface Wambura ilieleza kwamba viingilio katika mchezo huo, vilikuwa ni sh. 15,000, sh. 7,000, sh. 5,000 na sh. 3,000.
“Kutokana na viingilio hivyo sh. 23,388,000, zilipatikana ambapo kama inavyojulikana lazima zitolewe gharama za uwanja, chama cha soka mkoa na mambo mengine na kiasi kinachobaki hugawanywa kwa timu,” ilieleza sehemu ya taarifa hivyo.
Mbali na hilo, taarifa hiyo ya Wambura ilieleza kwamba
ili kutekeleza maagizo ya Serikali kucheza mechi mbili za ligi hiyo kwenye uwanja huo, shirikisho hilo limefanya marekebisho kwa baadhi ya mechi zilizokuwa zichezwe kwenye uwanja huo.
Alisema mechi zitakazochezwa katika uwanja huo ni Azam dhidi ya Yanga, itakayopigwa Septemba 18, Simba na Mtibwa Sugar itacheza Septemba 25, Yanga na Coastal Union zitaumana Septemba 28 na Yanga dhidi ya Kagera Sugar Oktoba 13.
Wambura alisema mechi zingine ni Simba itakayoumana na African Lyon Oktoba 16, Yanga itaikaribisha Toto African Oktoba 20, Simba itaivaa JKT Ruvu Oktoba 22, Yanga itacheza na Simba Oktoba 29 na Moro United itaikaribisha Simba Novemba 2, mwaka huu.
Alisema mechi zingine zitachezwa Uwanja wa Azam uliopo Chamazi ambazo ni Simba na Polisi Dodoma Septemba 14), African Lyon itaikaribisha Yanga Septemba 15, Yanga itaumana na Villa Squad Septemba 21, Simba itaumana na Ruvu Shooting Oktoba 19 na Yanga na Oljoro JKT Oktoba 23.
Iliongeza kwamba uongozi wa Azam unaomiliki uwanja huo, tayari umekubali timu za Simba na Yanga kutumia uwanja huo kwa mechi hizo.
No comments:
Post a Comment