12 September 2011

Simba ulimi nje kwa Azam

*Yalazimishwa suluhu, yaongoza ligi

Na Zahoro Mlanzi

LICHA ya timu ya Simba kuonja joto ya jiwe kwa mara ya kwanza tangu Ligi Kuu ya Tanzania Bara kuanza msimu huu kwa kutoka suluhu na Azam FC, katika mchezo
uliopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam jana, imekaa kileleni mwa ligi hiyo.

Kwa matokeo hayo, Simba imeshika usukani kwa kufikisha pointi 10, mbele ya JKT Ruvu yenye pointi tisa ikiwa katika nafasi ya pili na Azam ina pointi nne na kupanda mpaka nafasi ya nane.

Katika mchezo huo, Azam ina kila sababu ya kujilaumu kutokana na nafasi nyingi walizotengeneza, lakini washambuliaji wao walioongozwa na John Bocco 'Adebayor', hawakuwa makini kukwamisha mpira wavuni.

Kipindi cha kwanza, Azam walitengeneza nafasi tatu za wazi, kama Bocco angekuwa makini, hakuna shaka katika mchezo huo angeweza kuondoka na mpira kwa kuifungia timu yake mabao zaidi ya matatu.

Sekunde ya 45 tangu kuanza kipindi cha kwanza, Azam walifanya shambulizi la nguvu langoni mwa Simba, lakini Bocco aliunganisha vibaya krosi ya Ramadhani Chombo 'Redondo', akiwa ana kwa ana na kipa Juma Kaseja.

Ni Bocco tena dakika ya saba aliyeunganisha krosi ya beki Wazir Omari, ambaye mpira wake ulitua mikononi mwa Kaseja, kitendo ambacho mashabiki wa Azam walianza kupiga mayowe kuashiria kukerwa na kukosa mabao ya wazi kwa mshambuliaji huyo.

Simba ilitulia na kufanya shambulizi la kushtukiza dakika ya nane kupitia kwa Gervais Kago, ambaye aligongeana pasi vizuri na Amir Kiemba, lakini alichelewa kuuwahi mpira na kipa Mwadini Ali aliuwahi na kuudaka.

Ikiwa imebaki dakika moja kabla ya mapumziko, Bocco nusura aifungie timu yake bao, baada ya kuunganisha kwa kichwa mpira uliopigwa na Kipre Tcheche na kupaa juu ya goli.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi, huku Azam ikionekana kutawala mchezo zaidi, ambapo dakika ya 73, Ibrahim Mwaipopo alipiga faulo iliyogonga mwamba wa goli na kurudi ndani, lakini mabeki wa Simba waliondosha hatari.

Azam waliendelea kuliandama lango la Simba, hasa ikionekana kutakata zaidi eneo la kiungo, ambalo lilikuwa chini ya Mwaipopo, Jabir Aziz na Redondo,  ambao walionekana kuwazidi maarifa viungo wa Simba.

Simba ambayo ilikuwa imejaza viungo wengi, katika muda mwingi walitumia winga wao Ulimboka Mwakingwe na Kiemba kupitisha mipira, lakini ikifika katikati, ilinaswa na mabeki wa Azam na kuondosha hatari.

Azam itajutia nafasi aliyopata Bocco dakika ya 75, kwa kushindwa kuunganisha mpira wa kichwa uliopigwa na Wazir na dakika ya 88, Simba nayo kupitia kwa Uhuru Seleman aliyeingia badala ya Shija Mkina, ambaye naye aliingia badala ya Kiemba, kushindwa kufunga kutokana na shuti lake kutoka pembani ya goli.

Simba:Kaseja, Nassor Said, Amir Maftah, Juma Nyosso, Victor Coasta, Patrick Mafisango, Kiemba/Mkina/Seleman, Jerry Santo, Kago/Shomari Kapombe na Mwakingwe.

Azam:Mwadin Ally, Erasto Nyoni, Wazir Omari, Said Morad, Aggrey Morris, Mwaipopo, Mrisho Ngassa, Jabir Aziz, Bocco, Kipre/Wahab Yahya na Redondo.

No comments:

Post a Comment