Na Zahoro Mlanzi
MWAMUZI kutoka Mwanza, Alex Mahagi ameonekana kuikera Klabu ya Yanga kutokana na kudaiwa kushindwa kuzitafsiri sheria 17 za soka kwa kuipendelea
Ruvu Shooting.
Timu hizo zilikutana juzi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mfululizo wa michezo ya Ligi Kuu Bara, ambapo zilitoka sare ya bao 1-1.
Akizungumza mara baada ya kumalizika mchezo huo juzi uwanjani hapo, Ofisa Habari wa klabu hiyo Louis Sendeu, alisema timu yake kwa sasa hivi itakuwa makini na mwamuzi huyo (Mahagi), kwani anaonekana kutowatakia mema.
“Ni lazima tuchukue hatua za kisheria juu ya hilo ni dhahiri mwamuzi ameonesha mapenzi yake kwa timu fulani, ambayo tunajua kabisa ni shabiki mkubwa wa timu hiyo na ndiyo maana ameamua kuzidi kutunyong’oshesha, ili tusiende mbali.
“Hakufuata sheria 17 za uamuzi, lazima tuwajulishe TFF (Shirikisho la Mpirawa Miguu Tanzania) na chama chao (FRAT), ambapo tutawaomba wauangalie mchezo huo, ili kuona kama kweli alifuata kanuni katika kutoa maamuzi yake,” alisema.
Alisema mwamuzi huyo ndiye alichezesha msimu uliopita, dhidi ya African Lyon na pia mchezo huo timu hizo zilitoka sare, hivyo historia yake inaonesha dhahiri ana chuki na Yanga, lakini hivi sasa hawatakubali na ikiwezekana hawatakubali wachezeshwe na mwamuzi huyo tena.
Sendeu alisema kadi nyekundu ya Niyonzima (Haruna), aliyopewa haikuwa sahihi kwani aliwapiga chenga mabeki ndani ya eneo la hatari lakini wakamchezea faulo, katika jambo la kushangaza alioneshwa kadi ya pili ya njano na ikafuata nyekundu, huku mashabiki wakibaki wanashangaa kwa tukio hilo ambapo ilitarajiwa kutolewa penalti.
Akizungumzia mchezo ujao dhidi ya Lyon, Sendeu alisema ana uhakika Kocha Mkuu wa timu hiyo Sam Timbe, anazidi kuona upungufu wa timu yake hivyo atayafanyia kazi ili katika mchezo huo waondoke na pointi tatu.
Yanga kwa matokeo hayo, imebaki mkiani mwa ligi hiyo ikiwa na pointi tatu kutokana na michezo minne iliyocheza, ambapo ilifungwa na JKT Ruvu bao 1-0, ikatoka sare na Moro United ya bao 1-1 na kutoka suluhu na Mtibwa Sugar.
Sendeu wacha maneno mengi mdomoni,sasa tusubiri mchezo mwingine sijui utakuja na malalamiko gani.Timu imecheza mechi nane na haijashinda hata mechi moja alafu ndio inaitwa eti timu bora Afrika mashariki
ReplyDelete