*Ni baada ya kuiadhiri Coastal 5-0
Na Zahoro Mlanzi
UNAWEZA usiamini kilichotea Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam jana, au ukaona ni masihala, lakini ndio hivyo, mabingwa wa Ligi Kuu Bara, Yanga wamepata ushindi
mnono kwa mara ya kwanza tangu kuanza kwa ligi hiyo, baada ya kuiadhiri Coastal Union ya Tanga mabao 5-0.
Ushindi huo umewapa faraja kubwa mashabiki wa timu hiyo, ambayo kwa muda mrefu ilikuwa ikishindwa kufanya kile walichokuwa wakitarajia kutokana na kupata matokeo mabaya katika baadhi ya mechi.
Mashabiki hao ambao hawakuwa wengi kama ilivyozoeleka, mara baada ya kumalizika kwa mchezo huo, walionekana nje ya uwanja wakishangilia kwa nguvu huku wakiimba Simba! Simba! Simba!.
Kwa ushindi huo, Yanga imepiga hatua kubwa kwa kupanda mpaka nafasi ya nne, kwa kufikisha pointi 12, sawa na timu za JKT Ruvu na Mtibwa Sugar, lakini zinatofautiana kwa mabao ya kufunga na kufungwa.
Yanga ina tofauti ya mabao matano, wakati JKT ina mabao manne zikiwa sawa, na nafasi ya tatu inashikiliwa na JKT Oljoro ikiwa na pointi 13, huku Azam na Simba, zikikaa kileleni.
Katika mchezo huo, karamu ya mabao ilianza dakika ya nne, baada ya Keneth Asamoah kufunga bao kwa kichwa, akiunganisha krosi ya nzuri Idrisa Rashid, ambaye katika mchezo huo alionekana kutakata zaidi.
Yanga iliendelea kuliandama lango la Coastal Union, na dakika ya 22, Shamte Ally alifunga bao la pili akimalizia krosi iliyopigwa na Asamoah.
Baada ya kufungwa mabao hayo, Coastal ilionekana kupoteana, hasa eneo la kiungo na dakika ya 28, Ramadhan Nyumbi wa Coastal alitolewa na kuingia Said Swed kutokana na upande wake kuonekana kuzidiwa.
Mabadiliko hayo hayakusaidia kwani dakika ya 30, Davies Mwape, alifunga bao la tatu akimalizia mpira uliotemwa na kipa Omari Hamis kutokana na shuti lililopigwa na Idrisa.
Zikiwa zimebaki dakika nne kipyenga cha mapumziko kupulizwa, Nurdin Bakari aliifungia Yanga bao la nne, baada kuanzisha mashambulizi na kutoa pasi kwa Haruna Niyonzima aliyempigia Asamoah, kabla ya kurudishwa kwa Nurdin na kufunga.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi na dakika ya kwanza, Asamoah alifunga bao la tano akiunganisha krosi iliyotoka kwa Idrisa, ambaye alikuwa mwiba kwa timu hiyo kutokana na kucheza kwa kujiamini na kupiga pasi zenye uhakika.
Baada ya kufungwa kwa mabao hayo, Yanga ilionekana kuridhika, ambapo katika dakika za 63 na 65 ilifanya mabadiliko kwa kuwatoa Mwape na Asamoah na kuwaingiza Rashid Gumbo na Hamis Kiiza, mabadiliko ambayo yaliounguza kasi ya Yanga.
Coastal ilionekana kama imeamka usingizi, ambapo ilianza kuliandama lango la Yanga na kama washambuliaji wao walioongozwa na Benard Mwalala mchezaji wa zamani wa Yanga wangekuwa makini, wangepata bao.
Dakika ya 75, Fransis Busungu wa Coastal nusura afunge bao, baada ya shuti lake akiwa ndani ya eneo la hatari, kutua mikononi mwa kipa Yaw Berko, akimalizia pasi ya Mwalala.
Zikiwa zimebaki dakika mbili kabla ya mpira kumalizika, Busungu aliwapunguza mabeki wa Yanga na kupiga shuti lililodakwa na Berko ambaye aliwapigia kelele mabeki wake.
Yanga:Berko, Shadrack Nsajigwa, Oscar Joshua, Bakari Mbegu, Nadir Haroub 'Canavaro', Nurdin, Shamte/Julius Mrope, Niyonzima, Mwape/Gumbo, Asamoah/Kiiza na Idrisa.
Coastal:Omar Hamis/Godson Mmasa, Nyumbi/Swed,Soud Juma, Mbwana Hamis, Jamal Machelanga, Mwinyi Abdulrahman, Busungu, Mohamed Ibrahim, Daniel Lianga, Mwalala na Rashid Mandawa.
No comments:
Post a Comment