29 September 2011

TFDA yakabidhiwa maabara ya kisasa

Na Gladness Mboma

WIZARA ya Afya na Ustawi wa Jamii na Shirika la Afya Duniani (WHO) imezindua maabara ya Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA),ambayo itakuwa na uwezo wa
kufanya uchunguzi wa aina nyingi za kimaabara na zenye ufanisi wa hali ya juu na kutoa matokeo ya kuaminika duniani.

Maabara hiyo itakuwa ni ya kwanza barani Afrika kwa taasisi za serikali za udhibiti wa bidhaa kupata hadhi hiyo.

Utambuzi huo unaifanya maabara ya TFDA kuwa ya sita katika bara la Afrika kutambuliwa na WHO na inakuwa ya 19 kutambuliwa na WHO duniani.

Akizungumza mara baada ya kuzindua maabara hiyo, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dkt.Hadji Mponda, alisema maabara hiyo ya uchunguzi wa dawa inatambuliwa na WHO tangu Januari 18, mwaka huu.

"Kwa lugha rahisi ni kwamba kuanzia Januari mwaka huu nchi yoyote duniani inaweza kutumia maabara ya TFDA kuchunguza ubora na usalama wa dawa ambapo majibu yake yatatambuliwa na kukubalika kimataifa."alisema.

"Jambo la kujivunia zaidi juu ya maabara hii ni kuwa na uwezo wa kufanya chunguzi za aina nyingi za kimaabara na zenye ufanisi wa hali ya juu na matokeo kuaminika duniani.

Uwezo huu wa maabara ni mafanikio makubwa katika kudhibiti ubora na usalama wa dawa na hasa dawa duni na bandia ambalo ni moja ya malengo makuu ya kuanzishwa kwa mamlaka hii,"alisema.

Alisema serikali inatambua kuwa ili kufanya maamuzi ya  haki na kwa haraka kuhusu usajili wa bidhaa ni muhimu kupata matokeo ya uchunguzi wa kimaabara yenye ubora na kuaminika.

Dkt. MPonda alisema kwa mantiki hiyo mafanikio hayo yataongeza imani ya wadau ikiwa ni pamoja na wananchi kuhusu ubora na usalama wa bidhaa.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa TFDA, Bw.Hiiti Silo, alisema mchakato wa kuhakikisha kuwa maabara ya uchunguzi wa dawa inatambuliwa na WHO ulianza Agosti 4, mwaka 2004 kufuatia tangazo la WHO kuzitaka maabara ambazo zingependa kutambuliwa zionyeshe nia hiyo.

No comments:

Post a Comment