02 September 2011

Yanga kupigania maslahi yao

Na Addolph Bruno

UONGOZI wa klabu ya Yanga umesema utapigana mpaka mwisho kutetea maslahi ya klabu hiyo ambayo yanataka kutapeliwa na watu wachache kwa kivuli cha
katiba iliyopitwa na wakati.

Yanga, imelipongeza Jeshi la Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam, kuishauri Kamati ya muda ya Yanga iliyoshinda kesi mahakamani, kumaliza suala hilo kupitia Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), badala ya mahakamani.

Kamati hiyo inayoundwa na baadhi ya wanachama wa klabu hiyo chini ya Mwenyekiti wao,  Salumu Ngereza, hivi karibuni ilishinda keshi mahakamani ya kupinga katiba iliyouweka uongozi wa sasa mahakamani kwa madai kuwa, ilikiuka katiba ya yao ya mwaka 1968 iliyokuwepo kabla ya kufanyiwa marekebisho 1998.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa Yanga, Selestine Mwesigwe, alisema uongozi ulipata barua Agosti 19, kutoka kwa kamati hiyo kuutaka uongozi uliopo utoke madarakani baada ya ushindi wa mahakama.

"Kamati hiyo ilipeleka nakala ya ushindi wao TFF, nyingine kwetu na nyingine kwa Kamanda wa Polisi kanda ya Dar es Salaam,  Suleimani Kova, kuomba msaada kuutoa uongozi uliopo madarakani tangu Agosti 17,  mwaka jana, lakini imeshauriwa kumaliza mambo ya soka kwa kupitia TFF na vyama vya mpira na sisi tunaunga mkono jambo hilo,” alisema.

"Sisi tumefanya jitihada za kuwasiliana na mahakama ambako pia tumepewa ufafanuzi wa kumaliza mambo hayo kimichezo, na kwa upande wetu bado tunalifanyia kazi kisheria mpaka tuone mwisho kupinga utapeli, unaotaka kufanywa," alisema Mwesigwe. 

Alisema ingawa jambo hilo bado ni pana, wamelipeleka kwa Mwanasheria Mkuu wa klabu hiyo, ambaye analifanyiwa kazi kupinga utapeli unaotaka kufanywa na watu wachache kwa klabu hiyo.

Alisema wanachama hao kufungua kesi mahakamani,  inaashiria kuwa, hawautambui uwepo wa TFF na Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA), na kwamba Yanga italifuatilia kisheria suala hilo.

Alisema waliofungua kesi hiyo sio wanachama halali wa Yanga kwa kuwa, hawana kadi za uanachama na kwamba, wamegundua kuna mbinu za kutaka kuitapeli Yanga kupitia katiba ambayo imepitwa na wakati.

No comments:

Post a Comment