01 September 2011

Magufuli kutumia FFU kubomoa nyumba

*Atapambana na wanaojenga hifadhi za barabara
*Asema hana simile kwa wote wanaojiita matajiri
*Asisitiza kuoneana aibu hakutatufikisha mbali

Waziri wa Ujenzi, Dkt. John Magufuli akizungumza na waandishi wa habari, Dar es Salaam jana ambapo pamoja na mambo mengine alisema sasa wizara hiyo itawatumia Askari Polisi Kikosi cha FFU kuwakamata watu wote wanatumia hifadhi ya barabara kwa shughuli zao binafsi.

Na Benjamin Masese

WAZIRI wa Ujenzi Dkt. John Magufuli anatarajia kufanya oporesheni kali kwa kutumia kikosi cha kutuliza Ghasia (FFU) kupambana na
watu waliojenga nyumba, gereji, vituo vya mafuta, kufanya biashara, kuegesha magari katika hifadhi za barabara wakati wa ubomoaji wa majengo hayo.

Pia amesema pia ataanzisha mapambano dhidi ya watu wanaojiita matajiri na kiburi cha kutofuata sheria zilizowekwa na kusainiwa na Rais katika kuendesha shughuli zao kwa kuwa nyimbo za malaika alizoimba zimekwisha na sasa kilichobaki ni kutumia sheria.

Alisema hayo jijini Dar es Salaam jana wakati akizungumza na wandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru katika sekta ya ujenzi yanayofanyika kwa wiki moja kuanzia leo pamoja na kuelezea mafanikio yaliyopatikana tangu Tanganyika ipate uhuru mwaka 1961.

Mbali na maadhimisho hayo alisema kuanzia Septemba 5 hadi 7 mwaka huu Rais Jakaya atakutana na wakandarasi wote nchini, wadau wa ujenzi kutoka nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) kuzungumzia sekta ya ujenzi.

"Nimeimba nyimbo zote za malaika za kuwataka hawa wanaojenga katika hifadhi za barabara sambamba na wale wanaofanya biashara, kuegesha magari, wauza mbao, gereji, mabango, vituo vya mafuta sasa nimechoka na nimeishiwa nyimbo zilizobaki ni nyimbo za sheria.

"Tayari nimefanya mazungumzo na IGP na Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani wote wamekubali kunipatia askari kutoka FFU na wale wa usalama wa barabarani. Operesheni kali itaanzia mkoa wa Dar es Salaam wakati wowote, wananchi wakae mkao wa kufuata sheria la sivyo ukikamatwa umepaki pasipotakiwa faini ya papo kwa papo sh. milioni moja," alisema.

Dkt. Magufuli alisema kuwa watendaji wa sasa wamekuwa watu wa ajabu sana kutokana na kushindwa kufuata sheria na kusababisha wananchi wa kawaida kufuata mkumbo hali inayoashiria nchi kutaka kurudi enzi za ukoloni na kuwataka kufuata sheria ya mwaka 1977 ibara ya 26 kifungu cha kwanza na pili ambacho kinamtaka raia yeyote kuwa na wajibu wa kulinda katiba na sheria.

Pia alisema kuwa sheria inamtaka kila mwananchi kuheshimu hifadi za barabara huku akisisitiza watu kufuatilia historia za sheria za nchi ilivyokuwa tangu enzi za ukoloni mpaka sasa.

Dkt. Magufuli alisema kuwa sheria zikifuatwa na kila kiongozi na mwananchi bila kulindana na kuogopana, nchi itapata maendeleo makubwa na ya haraka kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali inayoibuliwa pia itaendelea kuwa kisiwa cha amani miaka 50 ijayo.

"Tukiendelea kupiga kelele za kuoneana aibu hatutafika mbali lazima tufanya maamuzi kama yaliyofanyika Kenya. Kenya majengo marefu yaliangushwa lakini hapa Tanzania ukitaka kubomoa sheli utakiona, watu wanaibuka kutetea maovu na kusimamia kesi mahakamani, itakumbukwa mwaka fulani tulishitakiwa kwa kubomoa nyumba lakini huyo watendaji walioko serikalini leo ndio waliosimamia kesi ya walalamikaji. Sasa tutafika,"alisema.

Alisema kuwa kutokana na sheria kufuatwa jumla ya wakandarasi 2,008 wamefukuzwa kazi na kufutiwa leseni ya ujenzi akiwemo aliyesimamia ujenzi  Barabara ya Kilwa ambayo inatarajiwa kurudiwa upya na tayari ubalozi wa Japani umewaomba radhi Watanzania.

Dkt. Magufuli alisema kuwa jumla ya wakandarasi 14,000 nchini wamesajiliwa na kati ya hao 7,000 ni wazalendo na kuongeza kuwa ataendelea kufuatilia mmoja baada ya mwingine katika utendaji wao wa kazi ili kubaini udhaifu wao na kuwafutia leseni.

Akizungumzia mafanikio yaliyopatikana tangu uhuru katika sekta ya ujenzi alisema hakuna asiyeona kuwepo kwa mabadiliko ya maendeleo ambapo hali halisi inajionesha katika barabara, nyumba za serikali na huduma za ufundi na vivuko.

Dkt. Magufuli alisema juhudi zilizofanywa na serikali zimewezesha mtandao wa barabara kupanda kutoka kilomita 33,600 zilizokuwepo mwaka 1961 hadi kufikia kilomita 86,472 mwaka 2011.

Alisema mafanikio katika sekta ya barabara yameleta mchango mkubwa katika kuinua uchumi wa taifa kwa jumla na kuongeza kuwa sekta nyingi zinafanya kazi kwa kutegemea barabara.

Pia alisema kuwa wakati Tanganyika inapata uhuru, serikali ilikuwa na magari yaliyosajiliwa 38,000 yakiwemo ya serikali na watu binafsi lakini sasa yanakadiriwa kuwa zaidi ya milioni 1.5 huku watu wakiwa milioni 9.54 ambapo leo ni zaidi ya milioni 40.

Alisema wakati huo barabara zilizokuwa za lami zilikuwa kilomita 1,300 sasa ni kilomita 6,500 na zinazotarajiwa kumailika ni kilomita 11,154 na kufanya jumla ya kilomita 17,700 baada ya miaka mitatu. Pia vivuko havikuwepo lakini sasa vipo vivuko 23 na madaraja yamefikia 4,480.

Dkt. Magufuli alisema bajeti ya kwanza iliyotengwa katika sekta ya ujenzi ikiongozwa na Waziri BwAmir Jamal (1961-1963) ilikuwa sh.bilioni mili lakini sasa sh.trilioni
1.496.

Hata hivyo Dkt.Magufuli alizungumzia miradi ya maendeleo inayoendelea ikiwemo ujenzi wa barabara za juu, mabasi yaendayo kasi (DART), ujenzi wa Daraja la Kigamboni, Mifuko ya Barabara, Wakala wa Ufundi na Umeme, Wakala wa Majengo, Usalama wa Barabara na Mazingira, sera na sheria.



1 comment:

  1. jamani kwanini nyie viongozi hamjifunzi kutoka kwa wenzenu libya, misri na tunisia.

    ReplyDelete