02 September 2011

Waziri Simba atangaza kushughulikia asasi

Na Benjamin Masese

WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto Bi. Sophia Simba, amezitangaza kiama dhidi ya taasisi na mashirika yote nchini yaliyosajiliwa kuwasaidia watoto yatima na
  wanaoishi mazingira magumu, huku yakijipatia fedha pasipo kutekeleza malengo hayo.

Pia amesema Tanzania haijafikia hatua ya kushindwa kuwahudumia watoto wanaoishi katika mazingira magumu kulingana na rasilimali zake.

Badala yake amewataka viongozi au wananchi mwenye huruma kujitolea kwa kuchukua mtoto mmoja na kuishi naye ndani ya familia.

Hayo aliyasema Dar es Salaam jana na Bi.Simba alipotembele Kituo cha kulelea watoto wanaoishi katika mazingira magumu cha New Hope Family Street Children na kujumuika nao kusherehekea sikukuu ya Idi el Fitri, ambapo alitoa msaada wa vitu mbalimbali vyenye thamani ya sh. 800,000 na kuendesha  harambee iliyofanikisha kupatikana sh.310,400.

Bi. Simba alisema kumekuwepo na baadhi ya asasi  nchini kujisajili kwa ajili ya kusaidia watoto yatima na wale wanaoishi katika mazingira magumu na kutumia mgongo wao kuomba fedha kutoka serikalini, mashirika makubwa na mabenki, lakini baada kupata fedha zinatokomea pasipojulikana.

Alisema dawa ya taasisi hizo za mfukoni tayari ipo jikoni, ambapo  kikosi kazi kimeanza kufanya utafiti kwa kuzifuatilia ili zichukuliwe hatua za kisheria.

"Muda umefika mwisho wa NGos za mfuko kutumia jina la watoto yatima na kujipatia mamilioni ya pesa na kutoweka huku zikiwatelekeza watoto hao, tayari kikosi kazi kipo kinazifuatilia ili kubaini utendaji wake," alisema.

Alisema Tanzania haijafikia hatua ya kushindwa kuwaondoa watoto mitaani.

Bi. Simba alisema kumeibuka vitendo vya akina mama kuwachukua watoto wao kwenda kuomba barabarani bila sababu huku wao wakikaa pembeni kusubiri makusanyo.

"Hawa akina mama wamekuwa wasumbufu katika vituo vya kulelea watoto, tumeishajua ni njama zao za makusudi kuwafanya watoto wao kama mtaji wa kimaisha, kitendo hicho ni kosa la jinai wanapaswa kuhumiwa kifungo lakini kutokana na haki za binadamu na hali halisi ilivyo nchini pengine tunawasamehe, lakini nao watashughulikiwa,"alisema.

Naye Mwanzilishi na mwenyekiti wa kituo hicho, Bw. Omar Kombe, ambaye alikuwa mtoto wa mitaani takribani miaka 12 alisema kuwa changamoto wanazokabiliana nazo ni pamoja na kukosa makao ya kudumu kwa watoto hao kwani kila mwaka hulazimika kulipa kodi ya pango sh. milioni mbili.

1 comment:

  1. Mh. Simba kama kweli upo serious na umeweka kikosi kazi nenda Karatu , kuna kituo kinaitwa Shalom, hapa ndio utaona madudu, kituo hicho kinamilikiwa na Mtu na mke wake Mr&Mrs.Nnko , hakina bodi ila ni majina hewa wafadhili wanapewa acc,iliyopo NBc wakati huo huo wamefungua acc, nyingine Exim, kwa hiyo wale wanaoweka kwenye acc,ya Nbc haifahamiki zinakwenda wapi na za Exim matumizi binafsi, kuna Mzungu mmoja alishawahi kufanya kazi ya kujitolea alipoanza kuhoji matumizi ya pesa,alichokipata hatawahi kusahau na alilazimika kurudi kwao baada ya vitisho vya kuuawa na kupewa kesi hewa,

    ReplyDelete