02 September 2011

Diwani wa CHADEMA Kirumba afariki

Na Daud Magesa,Mwanza

CHAMA Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Jijini Mwanza kimepata pigo baada ya diwani wa Kata ya Kirumba, Bw. Manoko, kufariki dunia.Taarifa zilizopatikana
na kuthibitishwa na Katibu wa CHADEMA  Mkoa wa Mwanza  Bw.Wilson Mushumbusi, zilieleza kuwa kuwa diwani huyo alifariki jana saa moja usiku katika
Hospitali ya Rufaa ya Bugando alikokuwa amelazwa.

Akizungumza nagazeti hili kwa simu, Bw.Mushumbusi alisema  kifo cha diwani huyo kilisababishwa na homa ya mapafu.

"Majira ya saa kumi jioni jana nilikwenda kumjulia hali, lakini nilimkuta akiwa na hali mbaya.Alikuwa akisidiwa kupumua kwa msaada wa mashine,tatizo hilo lilimpata
juzi," alisema.

Alisema saa moja jioni baada ya kutoka kumjulia hali alipokea taarifa kutoka kwa ndugu zake kuwa amefariki baada ya hali yake kubadilika ghafla.

Alisema mipango ya mazishi ya diwani huyo
inafanywa na ndugu zake kwa kushirikiana na uongozi wa mkoa wa CHADEMA na kuwa taarifa rasmi zitatolewa ni lini atazikwa.

Bw. Mushumbusi alisema chama hicho kimepata pigo hasa kutokana na jinsi alivyokuwa mchapakazi.

"Hakika CHADEMA imepata msiba mkubwa wa kuondokewa na mmoja wa viongozi wachapa kazi,pengo lake si rahisi kuliziba,ninapenda kuwapa pole wananchi wa kata ya
Kirumba kwa kuondokewa na mwakilishi wao,",alisema Bw.Mushumbusi.

Marehemu Manoko alichaguliwa kuwa diwani wa CHADEMA katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2010,akiwashinda wapinzani wake, Bw.Nuru Mohamed (CCM) na mgombea wa TLP, Bw Kisyeri.

Kabla ya kujiunga na CHADEMA, Bw. Manoko alikuwa ni mwanachama wa CCM na aligombea udiwani na kushindwa katika kura za maoni ndani ya CCM .Kutokana na kutoridhishwa na
matokeo ya kura hizo aliamua kutimkia CHADEMA na kuibuka na ushinda.

No comments:

Post a Comment