Na Gladness Mboma
MWANASHERIA ambaye pia ni mwanaharakati, Bw. Kainerugana Msemakweli ameibuka tena na kutaja majina ya watu sita ambao anadai kwa kupitia Kampuni ya
Kagoda Agriculture Limited walitumiwa kuchota mabilioni ya fedha kutoka katika Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA).
Bw. Kainerugana aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana kuwa tayari nyaraka anazodai ni za wizi wa fedha hizo ameziwasilisha kwa Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP) Bw. Eliezer Feleshi kwa hatua zaidi.
Katika orodha hiyo (majina tunayo) wapo wafanyabiashara maarufu na wanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) ambapo anadai alifuatilia kwa karibu sakata la wizi wa fedha hizo za umma kwa kipindi cha miaka miwili sasa.
Akionyesha vielelezo na ushahidi kibao ambavyo andai vilitumika katika sakata hilo zima la wizi wa fedha hizo za EPA alidai katika kufuatilia suala hilo alifanikiwa kukusanya na kufahamu ushahidi ambao unawaunganisha moja kwa moja watuhumiwa hao aliowataja na wengine katika wizi huo.
"Mimi niko tayari kuthibitisha tuhuma hizi katika mahakama yoyote sionei mtu yoyote vielelezo vyote ninavyo wezi wa fedha za EPA ni hawa niliowataja,"alisisitiza.
Alisema kuwa amekwishampelekea ushahidi DPP wa wizi huo wa fedha wa sh. bilioni 330 Jumanne ya wiki hii na DPP alimtafuta juzi na kumpongeza kwa kazi aliyofanya na kumuahidi kuonana naye leo asubuhi kwa mazungumzo zaidi.
Bw. Msemakweli alisema inashangaza watuhumiwa wote wanajulikana na tayari walikwisharejesha fedha hizo lakini serikali imekaa kimya bila ya kuwakamata na kuwafungulia mashtaka na badala yake wako nje wanatanua watakavyo.
Alisema Agosti 21 mwaka 2008 Rais Jakaya Kikwete katika hotuba yake kwa Bunge alisema baada ya jitihada za kukusanya fedha zilizoiibiwa sheria itachukua mkondo wake.
Bw. Msemakweli alisema kama alivyoahidi Dkt. Kikwete muda mfupi baada ya hotuba yake yeye na Watanzania walishuhudia watuhumiwa wakikamatwa, kushtakiwa na kufikishwa mbele ya mahakama kujibu tuhuma za wizi wa fedha za EPA.
"Matumaini ya awali ya Watanzania kwamba sheria itachukua mkondo wake yaliingia dosari pale ilipoonekana kwamba walioko nyuma ya Kagoda Agriculture Limited ambayo ndiyo iliyoiba fedha nyingi kuliko kampuni ya mtu yoyote hawakufikishwa mahakamani.
Alisema Rais kwa usikivu wake alijitokeza na kuondoa hofu umma kwamba uchunguzi ulikuwa unafanyika ndani na nje ya nchi mara tu baada ya kukamilika kwa uchunguzi huo watuhumiwa waliohusika na wizi wa Kagoda wangefikishwa mbele ya sheria.
Bw. Msemakweli alisema hivi karibuni matumaini ya Watanzania kwamba haki itatendeka katika suala hilo yamepotea baada ya Rais kunukuliwa kwenye vyombo vya habari akisema hakuna ushahidi dhidi ya mtu yoyote kuhusiana na wizi wa Kagoda na badala yake kuomba ushahidi kutoka kwa umma, msimamo ambao ulirudiwa tena na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ndani ya kikao cha Bunge kilichopita.
"Katika kufuatilia suala hili mimi nimefanikiwa kukusanya na kufahamu ushahidi ambao unawaunganisha moja kwa moja watuhumiwa hawa sita na wengine katika wizi huo,"alisema.
Alisema kwa kuzingatia kwamba kwa muda mrefu Watanzania wamekuwa wakizungumzia na kusikiliza suala hilo hata kuacha kufanya shughuli za maendeleo, ameitikia wito wake wa kupeleka ushahidi kwake unaowahusisha moja kwa moja watuhumiwa hao.
Thanks Msema kweli nilikuwa sielewi kitu thanks we ni mwanaharakati wa kweli.
ReplyDeleteHUO NDIO UZALENDO YAANI YUKO TAYARI KWA LOLOTE LAKINI MSG SENT. NAOMBA MWANASHERIA NA WENGINE WOTE WANAOHUSIKA KULIFANYIA KAZI SUALA HILI. TUACHE KULINDA KWA MAMBO MAZITO KAMA HAYA.
ReplyDeleteBravo Msemakweli. Walao watano kama weye haki ya mama tanzanua ingekwamuka kwenye umasikini. Nnaomba wote mloguswa kufanya harambee msemakweli alindwe kwani tayari alowafichua ni maadui wa wote na hasa MSEMAKWELI ambaye ni mzalendo KWELI KWELI!!!!.
ReplyDelete