Na Mwandishi Wetu
WANAMUZIKI wa zamani na wa kizazi kipya, wanatarajia kuungana kuimba jukwaa moja Desemba 8, mwaka huu katika mkesha wa miaka 50 ya Uhuru.Katika onesho
hilo, wanamuziki wa zamani wataimba nyimbo za wasanii wa kizazi kipya na pia wasanii wa sasa nao wataimba nyimbo za zamani.
Akizungumza Dar es Salaam jana Mwenyekiti wa Sauti za Kale Waziri Ally, alisema wanatarajia siku hiyo kutakuwa na burudani ya kukata na shoka kwa kuwa kutakuwa na muziki wa zamani na wa kisasa.
“Hakika itakuwa burudani ya aina yake kwa mashabiki na Watanzania kwa ujumla, kwani muziki utakaotoka hapo utakuwa na ladha ya ina yake,” alisema Mwenyekiti huyo.
Alisema katika onesho hilo, wao wakongwe wamepania kuwaonesha wanamuziki wa sasa, kwamba wao wanaujua ujana na uzee pia huku wanamuziki wa sasa wakiwa wanajua ujana na si uzee.
“Sisi wote tuna lengo moja la kuungana na kupanga nini tunataka kufanya katika onesho hili la miaka 50 ya Uhuru, litakalorindima Diamond Jubilee,” alisema.
Naye mwanamuziki nguli nchini King Kikii, alisema siku hiyo patakuwa hapatoshi katika burudani hiyo, kwani wanajiandaa kuhakikisha wanakumbushia enzi za zamani ambapo mazoezi yataanza wiki ijayo.
No comments:
Post a Comment