Na Sammy Kisika, Mpanda
VIONGOZI wa Chama cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Mpanda mkoani Rukwa (MUFA), wametishia kujiuzulu nyadhifa zao kwa madai ya kuingiliwa utendaji kazi
zao na uongozi wa wilaya hiyo.
Katika barua yao
waliyouandikia uongozi wa chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Rukwa (RUREFA), viongozi hao
wamedai kuchoshwa na maamuzi ya Kamati ya Michezo ya wilaya hiyo kuingilia kazi zao, kiasi cha kuwakatisha tamaa kiutendaji.
Katibu wa MUFA, Evarist Ntinda,
alisema kuwa, yapo mambo mengi ambayo uongozi wao hautendewi haki na
Kamati ya Michezo, ikiwemo kusimamisha ligi ya kusaka vipaji
iliyoandaliwa na chama hicho kwa kuzishirikisha timu za wilaya ya Mpanda Mjini na Mpanda
vijijini.
Ntinda alisema hawaelewi ni vipengele
gani vilivyozingatiwa kusimamisha ligi hiyo, ambayo ilidhaminiwa na
mfanyabiashara mmoja na kuitwa ligi
ya Louis.
Alisema tatizo lilitokea
baada ya Kamati ya Utendaji ya MUFA kuzionya baadhi ya timu na kuziengua kwenye mashindano hayo timu mbili za Kakese FC na TRL ya Katumba, baada ya kubainika kupanga matokeo katika mchezo wao wa mwisho.
Malengo yao ya kupanga matokeo katika mechi yao, inadaiwa ni kutaka kuinyima nafasi Makanyagio FC ya Mjini Mpanda.
“Baada ya maamuzi ya kamati,
tulipokea maagizo kutoka Baraza la Michezo la Wilaya likituamuru tusimamishe ligi kwa madai kuwa, timu hizo zimekata rufaa kwao, tulishangaa ni kwanini
zikate rufaa baraza, badala ya kamati ya mashindano?” Alihoji
Ntinda.
Katibu huyo alisema tatizo
kubwa lililopo katika Kamati hiyo, ni kuongozwa kiutendaji na
viongozi wa MDFA, ambao wanadaiwa kuhusika kumshawishi Katibu Tawala kusimamisha ligi hiyo.
“Tumejitahidi kutafuta wadau wa kusaidia maendeleo ya soka kwa kuanzisha ligi ambayo ingefanyika kila mwaka, lakini kwa maamuzi kama haya, hatuwezi kuendelea kabisa, tumewaomba RUREFA kuingilia kati suala hili, vinginevyo tujiuzulu nyadhifa zetu.”
Kwa upande wake Mwenyekiti wa MDFA,
Emmanuel Chaula, alisema tatizo la MUFA ni kutofahamu taratibu za kuendesha mchezo huo na kwamba mambo
mengi yanafanywa kwa jazba, badala ya kuzingatia taratibu zilizopo.
"Ni kweli MDFA tuliomba
kamati ya michezo ya wilaya iingilie kati suala la timu mbili kuenguliwa
katika hatua ya Sita Bora, kwanza MUFA haikuwa na ushahidi wa upangaji
matokeao katika mchezo huo uliomalizika kwa Kakese FC kukubali kipigo cha mabao 4-1 dhidi ya TRL Katumba.
Mashindano hayo ya kombe la Louis
yamedhaminiwa na mfanyabiashara Joachimu Louis, aliyetoa zawadi ya sh. 800,000 kwa mshindi kwanza, sh.500,000 kwa mshindi wa pili, wakati mshindi wa tatu sh. 300,000.
Michuano hiyo ilianza kuchezwa ikiwa na timu 15, na kutakiwa timu sita kuingia hatua ya sita bora.
No comments:
Post a Comment