*Kuweka ving'amuzi milangoni
Na Zahoro Mlanzi
KAMATI Maalumu ya Kudhibiti na Kuboresha mapato ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), imependekeza zitumike tiketi za eletroniki katika
mechi mbalimbali badala za karatasi na kuweka ving’amuzi milangoni, ili kuziba mianya ya upotevu wa mapato hayo.
Mbali na hilo, kamati hiyo pia imependekeza tiketi hizo ziuzwe na mawakala maalumu, ambao watapatikana kwa kutangaziwa zabuni ya wazi ili kila mwenye sifa ajitokeze, ambapo shirikisho hilo halitahusika na kuuza tiketi kama ilivyo sasa hivi.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa kamati hiyo ambaye pia ni Rais wa shirikisho hilo, Leodegar Tenga alisema baada ya mchakato wa muda mrefu katika kulifanyia uchunguzi suala hilo, wanashukuru wamefanikiwa kupata ufumbuzi yakinifu na hawana shaka kilichobaki ni utekelezaji wa mapendekezo yaliyotolewa na kamati.
“Tumeamua kuitoa rasmi ripoti ya kamati hii kwa wadau wetu wa mpira, ili kujua jinsi tulivyo na mzigo mkubwa katika kuliendesha soka hapa nchini, tofauti na watu wengi wanavyofikiria kwa kuona wepesi wa kufuatilia kiasi kilichokusanywa bila kutaka kujua mahitaji yaliyopo kwenye kuliendesha soka,” alisema Tenga.
Alisema ili kuondokana na matatizo ya mapato, kamati imependekeza zianze kutumika tiketi za eletroniki kwani ana imani tiketi bandia, hazitakuwepo tena.
Tenga alisema tiketi hizo pia zitasaidia kufanya uhakiki wa mapato kwa vile yatakuwa yakifahamika mara moja, kadri zitakavyokuwa zikiuzwa katika mechi mbalimbali.
Alisema ripoti hiyo, pia imebainisha upungufu uliopo katika miundombinu ya viwanja kwamba haifanani na dunia ya leo, hivyo Idara ya Ufundi ya shirikisho hilo itazungumza na wamiliki wa viwanja ambao ni serikali, CCM na baadhi ya manispaa ili kuboresha viwanja hivyo.
“Si miundombinu pekee, kamati pia imependekeza kuwepo kwa utaratibu mzuri zaidi na wa wazi, utakaofanikisha upatikanaji wa rasilimali watu inayoaminika katika kusimamia udhibiti wa mapato milangoni ambapo tutaoa zabuni kwa vikundi na kampuni kuwania nafasi hiyo,” alisema Tenga.
Alisema ukiangalia hivi sasa watu wengi wanaogopa kwenda uwanjani kutokana na ushabiki uliopo unaofanya wengine kukosa amani, hivyo wataboresha usimamizi wa nidhamu ya watazamaji, ili uvutie kwa kila mtu kwenda ikiwezekana na familia zao.
No comments:
Post a Comment