17 September 2011

Waliokufa Z'bar ni 1,741-Mbunge

Watatu wafikishwa kortini kwa ajali hiyo

Na Nyakasagani Masenza

MBUNGE wa Jimbo la Ziwani, mkoani Pemba kwa tiketi ya Chama Cha Wananchi (CUF), Bw Ahmed Juma Ngwali amedai kuwa idadi ya waliokufa katika ajali ya meli ya Mv Spice Islanders ni 1,741.


Akizungumza na waandishi wa habari jana kwenye Ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO), Dar es Salaam jana, Bw. Ngwali alibainisha kuwa meli hiyo ilikuwa na abiria zaidi ya 2,360, idadi ambayoo ni kikubwa kuliko uwezo wa meli hiyo.

Akionesha kuwa na uhakika na maelezo yake, Bw. Ngwali aliahidi kuwa iwapo itathibitika kasema uongo kuhusu idadi hiyo ya waliokufa katika ajali, yuko tayari kuachia ngazi.

"Ninachosema ndio ukweli ya jambo hili ulivyo, kama itabainika kuwa nimesema uongo, niko tayari kujiuzulu ubunge wa Jimbo la Ziwani, waliokufa ni wengi tofauti na idadi inayotajwa na serikali ya Zanzibar", anasema Bw. Ngwali.

Alisema kuwa alifanya utafiti kwa kuzungukia maeneo walikotoka waliokufa kwa kutumia usafiri wake mwenyewe na kwa msaada wa watu waliopoteza ndugu zao.

Alisema baada ya kutokea kwa ajali hiyo, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, alifanya ziara Kisiwani Pemba kuwafariji wafiwa na kuwapa pole waliopotelewa na ndugu zao, na kubaini idadi hiyo kubwa.

Katika maelezo yake kwa waandishi wa habari jana, Bw. Ngwali alisema idadi inaweza kuwa kubwa zaidi kutokana na idadi aliyotaja kuwa ya mikoa ya Pemba, ambayo haikuhusisha wakazi wa Unguja.

Bw. Ngwali alisema takwimu zilizotolewa na wakuu wa wilaya kwa Makamu wa kwanza wa Rais Maalim Hamad zimetofautiana kidogo, kwani waliokufa katika ajali hiyo ni watu 1,741.

Alitaja takwimu za waliokufa katika ajali hiyo kwa kila mkoa Kisiwani Pemba kuwa ni kama ifuatavyo. Koani ni watu 27, tofauti na 24 waliotajwa, Chakechake watu 146, Micheweni 367 na Wete 1,204.

"Mfano kwenye Jimbo langu la Ziwani watu waliopoteza maisha ni 84, ambapo wanawake ni 44 na wanaume 40, katika idadi hiyo watoto wenye umri kati ya miaka 16 ni 50, vichanga na mwanaume aliyefahamika kama Lujaima Omar Suleiman wa Kijiji cha Kwale, aliyepotea pamoja na mama yake", anasema Bw. Ngwale.

Alisema katika mchanganuo huo, Jimbo la Ziwani hususan Kijiji cha Ziwani ndicho chenye idadi kubwa ya waathirika wa meli hiyo, baada ya kupoteza watu 46, huku Kijiji cha Nyiapi kikiwa na idadi ndogo ya watoto wawili Khamis Ali Faki na Juma Kombo Hamad.

Bw. Kombo alisema katika suala kama hilo la vifo vya wananchi siasa haina nafasi, hivyo ameitaka serikali kusema ukweli kuhusu idadi kamili ya waliopoteza maisha na 619 waliookolewa.



Wakati huo huo Nahodha Msaidizi wa Meli ya Mv Spice Islanders iliyozama na kuua mamia ya abiria katika mkondo wa bahari eneo la Nungwi amefikishwa mahakamani na maafisa wawili wa bandari ya Malindi mjini Zanzibar.

Nahodha huyo Abdallah Mohammed Ali (30) mkazi wa Bububu amefikishwa
mahakamani na kusomewa shitaka lake mbele ya Mrajisi wa Mahakama Kuu Zanzibar
Bw. George Joseph Kazi wa mahakama hiyo.

Wengine waliofikishwa mahakamani hapo na kusomewa mashtaka ni Simai Nyange
Simai (27) mkazi wa Mkele na Yussufu Suleiman Issa (47) mkazi wa Kikwajuni
ambao ni maafisa wanaosimamia usalama wa abiria bandarini.

Bw. Simai ni afisa anayesimamia usalama wa Abiria kutoka Mamlaka ya Usafirishaji
Zanzibar (ZMA) na Yussuf ni afisa anayesimamia usalama katika bandari hiyo.

Mwendesha Mashtaka kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar Ramadhan
Nasib alisema washitakiwa hao wanashitakiwa kwa kusababisha vifo kwa uzembe.

Alisema  Septemba 9 mwaka huu, majira ya saa 3:30 katika bandari ya Malindi Zanzibar waliruhusu kupakiwa kwa mizigo na abiria kupita uwezo na kusababisha meli hiyo kushindwa kuendelea na safari na kuzama
katika mkondo wa Nungwi saa 8:00 usiku na kuua watu 203 waliokuwemo ndani ya meli hiyo.

Alisema kitendo hicho ni kinyume na kifungu 236 sheria namba 6 ya mwaka 2004, ambapo washitakiwa hao hawakutakiwa kujibu mashataka hayo hadi kesi hiyo itakapoanza kutajwa katika Mahakama Kuu.

Hata hivyo Mwendesha Mashtaka alisema upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na kuomba mahakama isitoe dhamana kwa washitakiwa kwa sababu za kiusalama.

Hata hivyo wakili anaewatetea washitakiwa hao Bw. Hamid Bwezeleni alisema kuendelea kuekwa rumande washitakiwa hao ni sawa na kuwaadhibu kabla ya hukumu.

Alisema kwamba hakubaliani na upande wa mashtaka wa kutaka wateja wake
wasipewe dhamana kwa sababu za kiusalama kwa vile kama watapelekwa rumande
na kukutana na watu walioathirika na vifo hivyo usalama wao utakuwa katika
mashaka zaidi na hawana uwezo wa kujihami.

“Unapokuwa nje unakuwa na usalama zaidi lakini rumande sijui ukimbile wapi
je utajificha katika friji, nyuma ya meza”, alisema wakili huyo.

Hata hivyo Mrajisi huyo alisema anakubaliana na upande wa mashtaka pamoja na
dhamana kuwa haki ya mshitakiwa lakini na uzito wa shitaka lazima uangaliwe
kabla ya mahakama kutoa uwamuzi kuhusiana na suala hilo. Alisema ombi la dhamana litapitiw ana mahakama na kutolewa uwamuzi
wake kesi itakapotajwa tena Septemba 19 mwaka huu.

Mshitakiwa mwengine aliyesomewa shitaka bila kuwepo mahakamani ni Nahodha wa
meli hiyo Bw. Said Abdallah Kinyanyite ambaye hajuulikani alipo hadi sasa.

Washitakiwa hao walifikishwa mahakamani asubuhi lakini walichelewa kusomewa
mashtaka yao na badala yake walisomewa mashatka yao saa 7:30 baada ya hati
ya mashtaka awali kukosewa na kurekebishwa.

Meli ya MV Spice Islanders ilizama katika eneo la Nungwi Septemba 10 mwaka
huu, na kusababisha vifo vya watu 203 na watu 619 kusalimika.

Meli hiyo ina uwezo wa kuchukuwa abiria 600 na tani 420 za mizigo hadi sasa
haijaopolewa baada ya wazamiaji kutoka Afrika Kusini kushindwa kufanyakazi
ya kuiopoa

5 comments:

  1. hawa ndio muhanga? vyombo vya usalama wa bandari, mamlaka ya bandari, wizara husika nk hawa ndio wa kupelekwa mahakamani. hii tabia ya kubebana iwacheni wazenji

    ReplyDelete
  2. kwanini waziri husika yuko madarakani?hiyo ni kashfa kwa wizara yake hawezi kuiepuka tunachukulia hatua wadogo tu huku kuna kundi tunaliacha

    ReplyDelete
  3. vipi kuhusu idadi mpya iliyotajwa na mbunge wa jimbo la ziwani? (mh Ngwali)au swala hilo linapuuziwa? ni vyema serikali ichukue hatua zaidi kuhusu idadi hiyo mpya iliyotolewa

    ReplyDelete
  4. Bila ya accountability, hatuwezi kupiga hatua. Roho za watu wengi zimepotea na serikali bado inasita ku-enforce international adopted standards kwa kuhofia maslahi ya wachache. Hili ni somo kwa wewe mpiga kura. Bila ya kuwajibishwa hawa, usalama na maisha yako upo hatarini

    ReplyDelete
  5. uzembe wa wat wachache umesababisha maafa makubwa kiasi kile. Na sisi abiria tuwemakin nahawa wanaotusafirisha.

    ReplyDelete