17 September 2011

Sitta: Tanzania ni Ujerumani ya Afrika Mashariki

Na Tumaini Makene

KAMA ambavyo nchi ya Ujerumani inavyonufaika katika Umoja wa Ulaya, kutokana na faida ya eneo lake la kijiografia, ndivyo Tanzania pia itanufaika na fursa zinazopatikana kwenye uhusiano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, iwapo itaamua kwa dhati kuwekeza katika reli ya kati, bandari na kutumia rasilimali adhimu ya ardhi, ambayo nchi hii inajivunia kuwa nayo ya kutosha, kulinganisha na majirani zake wote.


Pia imeelezwa kuwa, iwapo Tanzania itaweka mkazo katika matumizi sahihi ya ardhi na 'mazao' mengine yaliyo ndani na juu yake kama vile, madini ya makaa ya mawe, gesi na maji ambavyo ni kati ya vyanzo vya umeme wa uhakika vilivyopo nchini, miaka kumi ijayo pato la taifa litapatikana kwa nchi kuuza umeme nje ya nchi, kuongezea katika mazao ya biashara na chakula, yanayotegemewa sasa.

Tanzania inao uwezo wa kutumia ukubwa na ubora wa ardhi iliyo nayo na vyote vilivyo ndani na juu yake, kuzalisha chakula cha kutosha kuuza nje ya nchi, hasa wakati huu ambapo wataalamu wa masuala ya uchumi duniani, wameshatabiri kuwa katika miaka ijayo kutakuwa na mahitaji makubwa ya chakula na maji, pengine hata  kusababisha vita, kugombania 'rasilimali' hizo.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Uhusiano wa Afrika Mashariki, Bw. Samuel Sitta alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jana katika Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Julius Nyerere, mara baada ya kutoka safari yake ya kikazi mkoani Arusha na Kigali, Rwanda, ambako alihudhuria mikutano ya Baraza la Mawaziri na Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC). 

Alisema kuwa katika mikutano hiyo miwili tofauti, yalijadiliwa masuala manne, ambapo katika mkutano wa Baraza la Mawaziri wa EAC, uliofanyika Makao Makuu ya jumuiya hiyo, mjini Arusha, ulijadili juu ya ombi la nchi ya Sudan kujiunga na EAC, ambalo lilitumwa Juni 10, takriban mwezi mmoja kabla nchi hiyo haijagawanyika na kuzaliwa kwa Sudan Kusini.

Pia katika mkutano huo wa Arusha, Tanzania ilitiliana saini na Uganda juu ya mradi wa kuzalisha umeme utakaojengwa katika maporomoko ya Mto Kagera, eneo la mpakani mwa nchi hizo mbili, wenye uwezo wa kuzalisha Megawati 16, ukijulikana kwa jina la Mrongo-Kigagati, ambayo ni majina ya maeneo ulipo mradi huo, kwa Tanzania na Uganda.

"Juu ya Sudan kujiunga na jumuiya, kutokana na ushauri wa wataalam wa sheria za kimataifa, hatujalikubali ombi hilo moja kwa moja, tumepeleka ushauri wetu wa mawaziri kwa mkutano mkuu wa wakuu wa nchi wanachama, kwa kweli tumeona kuwa ukiikubalia Sudan kwa sasa kujiunga na jumuiya wakati mambo yao hayako sawa bado hata juu ya mpaka tu bado kuna utata, tutatumia muda kujadili amani badala ya maendeleo kwanza.


"Hivyo tukishirikiana kwanza na Sudan Kusini, ambayo tunasubiri tu ombi lake kwa maandishi, ndiyo unaweza kushirikiana na Kaskazini na ukaweza kuwaambia kuwa malizeni kwanza utata wa mpaka na Kusini, kisha muingie...la sivyo tutakaribisha mjadala na kutumia muda kujadili amani, kisha tutashindwa kujadili ujenzi wa reli, barabara, matumizi ya maji Ziwa Viktoria na mengine," alisema Bw. Sitta.

Juu ya suala la Mradi wa Umeme wa Mrongo-Kigagati, Bw. Sitta alisema kuwa baada ya kutiwa saini kwa mkataba wa mradi huo, ambao utakagharimu takriban sh. bilioni 20, zikiwa ni fedha za msaada kutoka Benki ya Afrika (ADB), suala la utekelezaji litakuwa mikononi mwa wizara husika za nishati, kutoka nchi zote mbili. Mradi huo, ambao ni mfano wa ushirikiano, utakuwa tofauti na Mradi wa Kabanga.

No comments:

Post a Comment