06 September 2011

Wafanyakazi waituhumu TICTS kwa unyanyasaji

 Na Nickson Mahundi

CHAMA Cha Wafanyakazi wa shughuli za Bandari (DOWUTA), kimeitaka serikali kuchukua hatua za kisheria dhidi ya Kampuni ya Kupakia na Kupakua
Makontena katika Bandari ya Dar es Saalam (TICTS) kwa kutowatendea haki wafanyakazi wake.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana Mwenyekiti wa chama hicho Bw. Edmund Njowoka, alisema Kampuni ya TICTS imekuwa ikikiuka kwa makusudi Sera ya Taifa ya Ajira badala yake inatumia ajira ya vibarua kupitia kwa mawakala na kuwalipa watanzania ujira mdogo.

Alisema TICTS haitaki kutoa ajira za kudumu hivyo unyanyasaji wa wafanyakazi kwa kufukuzwa  bila kulipwa mafao yao kwa muda waliokuwa kazini unaendelea pamoja na upotevu wa mizigo hivyo kuishushia hadhi badari ya Dar es Salaam kwa mataifa mengine.

"Tunaitaka Serikali kuchukua hatua za haraka kuichunguza na kuikemea TICTS kuacha kabisa vitendo hivi, kampuni hii inawanyanyasa wafanyakazi wa bandari kupitia mawakala wake,"alidai Bw.Njowoka.

Alisema kampuni hiyo imekuwa ikiingia mikataba mibovu na kampuni za ulinzi zinazoajiri walinzi wasio na sifa hivyo kusababisha upotevu wa mizigo unaopelekea wafanyakazi kutopandishiwa mishahara na kutumia fedha zao kulipa fidia ya mizigo iliyopotea.

Mwenyekiti huyo alisema TICTS imetenga asilimia  tano ya hisa zake kwa wafanyakazi zenye thamani ya sh. bilioni 16.5 na kuwataka wazinunue kwa mishahara yao duni hiyo kitendo ambacho ni kiini macho cha kuwahadaa watanzania.

Majira ilipomtafuta Msemaji wa Kampuni hiyo Bw. Ibrahim Kyaruzi, kujua ukweli wa madai hayo alisema hawezi kuzungumzia suala hilo kwa kuwa msemaji mkuu yuko safari.

 “Nimepokea simu kutoka katika vyombo vingi vya habari wakiniuliza juu ya suala hilo, lakini msemaji mkuu yuko safari, akirudi atalizungumzia,”alisema Bw. Kyaruzi.

No comments:

Post a Comment