06 September 2011

Manispaa ya Temeke kuboresha taaluma

Na Grace ndossa

HALMASHAURI ya Manispaa ya Temeke Mkoa wa Dar es Salaam, imeweka mikakati ya kuboresha taaluma katika shule za msingi kutokana na baadhi yake
kutofanya vizuri katika mtihani wa mkoa wa kupima uwezo wa wanafunzi (MOCK).

Akizungumza na Majira jana Kaimu Mkurugenzi wa manispaa hiyo Bw. Gasana Gastoni, alisema, wamepanga kutekeleza mkakati huo kupitia idara ya elimu ya msingi kwa kuimarisha miundombinu hususan majengo.

Alisema kwa kuanzia watamaliza maboma matatu,  vyumba vya madarasa, nyumba za walimu pamoja na kumalizia ujenzi wa vyoo vya shule ya msingi Mizimbani katika bajeti ya mwaka huu.

"Shule ya msingi mizimbani kitaaluma siyo nzuri sana mtihani wa mock mkoa uliofanyika juni, mwaka huu wanafunzi hawakufanya vizuri, kati ya wanafunzi 45 waliofanya mtihani wanafunzi 20 tu ndiyo waliofaulu kwa wastani wa asilimia 44,"alisema Bw. Gastoni.

Alitaja mkakati mwingine katika kuboresha taaluma kuwa ni kufanya majaribio ya masomo mbalimbali mara kwa mara pamoja na kufuatilia kwa karibu ufundishaji mashuleni.

Kuhusu upatikananaji wa maji na umeme mashuleni alisema suala hilo bado ni changamoto kubwa na kwamba shule nyingi za msingi na sekondari hazina huduma hizo na kwamba hata zilizobahatika zilipitia kwa wafadhili.

mwisho.

No comments:

Post a Comment