Na Amina Athumani
WADAU wa riadha wameutaka uongozi wa Chama cha Riadha Tanzania (RT), akiwemo Katib Mkuu wake Suleiman Nyambui, ujiuzulu kwa kuwa hakuna mafanikio yoyote
katika mchezo huyo.
Wakizungumza juzi katika hoteli ya Lamada, wakati wa mjadala wa michezo kuhusu matokeo mabaya ya michuano ya Mataifa ya Afrika iliyomalizika Maputo, Msumbiji Septemba 18 mwaka huu wadau hao walisema ipo haja ya viongozi hao kujiuzulu kwa kuwa hakuna changamoto yoyote wanayoifanya kuhakikisha wanafanya vyema kwenye michuano mbalimbali.
Akizungumzia suala hilo, Nyambui alisema hayo ni mawazo ya wadau na kamwe hawezi kuyazuia kwa kuwa kila mdau wa michezo, anayo nafasi ya kutoa maoni yake.
"Unajua ule ulikuwa ni mjadala, hivyo kila mmoja anatoa maoni yake, mimi siwezi kumzuia mtu kusema hisia zake hivyo suala la mtu kujiuzulu ni uamuzi wake binafsi na si kushinikizwa na mtu," alisema Nyambui.
Alisema kwa kuwa wanajiandaa na Uchaguzi Mkuu hakuna shaka kwa wadau kusubiri uchaguzi, ambao ndiyo unaoamua kuwaweka madarakani viongozi wanaoona wanafaa.
Uchaguzi Mkuu wa RT, unatarajia kufanyika Novemba mwaka huu baada ya kumalizika kwa chaguzi za vyama vya mikoa, ambavyo baadhi yao tayari vimeshapata viongozi wao.
Nyambui alisema vyama vya mikoa, ambavyo havitafanya uchaguzi vitakosa sifa ya kushiriki katika Uchaguzi Mkuu, pamoja na kukosa wawakilishi katika Mkutano Mkuu kama wanachama hai.
No comments:
Post a Comment