27 September 2011

Stars kuivutia kasi Morocco

Na Zahoro Mlanzi

KATIKA kuhakikisha 'Taifa Stars' inajiandaa vyema kuikabili Morocco, timu hiyo inatarajia kucheza mchezo wa kirafiki wa kimataifa ugenini, kabla ya kuumana na timu
hiyo Oktoba 9, mwaka huu.

Mchezo huo utakuwa ni mwisho katika Kundi D wa kuwania kufuzu kucheza fainali za Mataifa ya Afrika, zitakazofanyika mwakani katika nchi za Guinea ya Ikweta na Gabon.

Mbali na mchezo huo, siku hiyo pia kutapigwa mchezo mwingine wa kundi hilo, kati ya Jamhuri ya Afrika ya Kati na Algeria ambapo Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), limepanga hivyo ili kuepusha upangaji wa matokeo.

Kundi hilo linaongozwa na Morocco yenye pointi nane sawa na Afrika ya Kati, ila zinatofautina kwa mabao ya kufunga na kufungwa na Taifa Stars ikiwa katika nafasi ya tatu kwa pointi tano sawa na Algeria.

Akizungumzia maandalizi ya timu hiyo, Ofisa Habari wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Boniface Wambura alisema watahakikisha wanapata timu ya kucheza na Stars, kabla ya kuumana na Morocco ili kuiongezea nguvu timu hiyo.

"Kuialika timu kuja kucheza nyumbani kiukweli ni ngumu, hatuna muda wa kufanya hivyo ila tutajitahidi kupata timu tucheze nayo juu kwa juu wakati tunakwenda Marrech nchini Morocco," alisema Wambura.

Alisema endapo kama hiyo timu itapatikana itabidi Stars, iondoke nchini Oktoba 3 mwaka huu na ikishindikana itaondoka kama ilivyopangwa awali Oktoba 6.

Wambura alisema Kocha Mkuu wa timu hiyo, Jan Poulsen alishindwa kutangaza kikosi jana kutokana na kuwa na udhuru, lakini timu itaingia kambini kama ilivyopangwa awali kesho jijini Dar es Salaam.

Akizungumzia suala la wachezaji wanaocheza soka la kulipwa (Maproo), alisema tayari Poulsen alishawapa majina ya awali ya wachezaji hao na wameshaanza kuwatumia taarifa na baadhi ya timu zimeanza kurudisha majibu.

No comments:

Post a Comment